Oct 04, 2022 08:03 UTC
  • Raisi: Kuwaachia huru wafungwa wa Marekani ni ithibati ya nia njema ya Iran

Rais wa Iran amesema hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuwaachia huru wafungwa wawili wa Marekani wenye asili ya Iran inaonesha wazi nia njema ya taifa hili, na azma yake ya kutatua matatizo kwa njia ya mashauriano.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema hayo kwenye mazungumzo yake ya simu na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye amepongeza kitendo hicho cha Iran cha kuwaachia huru Bagher Namazi na mwanawe wa kiume, Syamak Namazi.

Rais Raisi ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kutumia uwezo wake athirifu kuzipatia ufumbuzi changamoto za kieneo na kimataifa.

Wawili hao wamegusia mgogoro wa Yemen, mbapo Rais wa Iran amesisitiza kuwa, Tehran imekuwa ikisisitiza juu kuondolewa mzingiro wa Yemen, kusitishwa vita sambamba na kutafuta suluhisho la mgogoro wa nchi hiyo kupitia mazungumzo ya makundi ya Wayemen wenyewe, bila la uingiliaji wa maajinabi.

Rais wa Iran amesema anatumai kwamba Katibu Mkuu wa UN ataishinikiza Saudi Arabia ifungamane na wajibu wake na kusitisha vita, na vilevile ikubaliane na ukweli kwamba, Wayemen wenyewe ndio wanaopaswa kuamua mustakabali wao.

Kwa upande wake, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu kwa misimamo yake ya kibinadamu katika kujaribu kutafutia ufumbuzi changamoto za kieneo na kimataifa.

Mbali na kuashiria mazungumzo yake na Rais wa Iran pambizoni mwa mkutano wa hivi karibuni wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Guterres amemhakikishia Sayyid Ebrahim Raisi kuwa, atafanya juu chini kuishawishi Saudia isimamishe vita dhidi ya Yemen. 

 

Tags