Oct 04, 2022 10:24 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu juu ya kuratibiwa kutoka nje fujo na ghasia za Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba muhimu katika hafla ya pamoja ya wanachuo wahitimu wa Vyuo Vikuu vya vikosi vya ulinzi hapa Iran kuhusiana na fujo na ghasi za hivi karibuni hapa nchini zilizoibuka kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei sambamba na kubainisha kwamba ghasia na fujo zilizoshuhudiwa hivi karibuni hapa nchini ziliratibiwa na kueleza kwamba, ghasia hizo zilikuwa zimeratibiwa kitambo nyuma; kwani wachochea machafuko walipanga kuibua ghasia na ukosefu wa amani hapa nchini tarehe 23 Septemba mwaka huu kupitia kuibua kisingizio kingine hata kama lisingekuwepo suala la kifo cha binti huyo kijana.

Kiongozi Muadhamu amesema: Ninasema bayana kabisa kwamba, ghasia hizi zilipangwa na kuratibiwa na Marekani na utawala ghasibu na bandia wa Kizayuni na kusaidiwa kwa hali na mali na mabwana zao na baadhi ya wasaliti raia wa Iran wanaoishi nje ya nchi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Marekani si tu inaipinga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bali inapinga Iran iliyo imara na iliyo huru. Ameongeza kuwa, viongozi wa Marekani wanaitaka Iran ile iliyokuwepo wakati wa zama za Pahlavi; ambayo ilikuwa ikitii amri na matakwa yao kama ng'ombe anayekamwa maziwa. 

Sisitizo la Kiongozi Muadhamu juu ya kupangwa na kuratibiwa nje ya nchi fujo na ghasia za hivi karibuni hapa Iran ni jambo linalofahamika bayana hasa kwa kutilia maanani uungaji mkono wa pande zote wa uistikbari wa dunia ukiongozwa na Marekani kwa wafanyafujo, kuwaongozwa na kutangaza utayari wa kuchukua hatua za kivitendo za kuwaunga mkono mkono wafanyafujo hao kama vile kuondoa vikwazo vinavyohusiana na intaneti.

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani ikiwa kinara wa kambi ya Magharibi siyo tu kwamba, sambamba na kuiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu kabisa katika kipindi cha uongozi wa Donald Trump imekuwa ikifuatilia utendaji wa kuzusha vurugu na ghasia za kijamii, bali kila mara imekuwa ikitumia visingizio mbalimbali kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran ambapo mfano wa wazi ni fitina na vurugu za mwaka 2009 zilizoibuka kwa kisingizio cha kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais. Marekani ilifanya kila iwezalo kuunga mkono na kuwashajiisha wafanyafujo na watu wachache hapa nchini waliokuwa wakifanya vitendo vya utumiaji mabavu na kuharibu mali za umma kama kuchoma moto benki, mabasi ya umma na kadhalika.

Mbali na Marekani, kuna utawala haramu wa Israel ambao kimsingi umetangaza wazi na bayana uadui wake dhidi ya taifa la Iran kutokana na kuwaua wasomi na wataalamu wa nyuklia wa Iran sambamba na kuendesha vitendo vya uharibifu katika vituo na taasisi za miradi ya nyuklia ya taifa hili. Israel imekuwa bega kwa bega na Marekani na kutumia kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini ili kufikia malengo yake ambapo imekuwa ikiwachochea waziwazi watu wachache wasaliti hapa nchini wanaofanya fujo. Kuhusiana na hili hatupaswi kusahau nafasi ya wasaliti wachache hapa ndani hususan makundi yaliyo dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yamekuwa yakitumiwa na maadui kutoka nje. Kuna ushahidi na nyaraka nyingi zinazoonyesha kwamba, fujo hizi ziliratibiwa hapo kabla na maadui kutoka nje na vibaraka wao kwa ajili ya kuzusha fujo na ghasia hapa nchini.

 

Kiujumla ni kuwa, ghasia na fujo za hivi karibuni nchini Iran zilizoibuka kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini, kwa mara nyingine tena zimewafanya maadui wa nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutumia hilo kama fursa ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran sambamba na kuwachochea wafanyafujo. Aidha makundi yaliyo dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu kama kundi la Munafiqin (MKO) na makundi yanayopigania kujitenga kama la Komala yakiongozwa na kupatiwa himaya na madola ya Magharibi hususan Marekani na utawala vamizi wa Israel yamefanya kila yawezalo kunufaika na matukio haya ili kufikia malengo yao yaliyo dhidi ya Iran.

Ahmad Vahidi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran sanjari na kubainisha kwamba, licha ya kuwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unakabiliwa na njama kubwa lakini umeweza kuvuka kwa uwezo kamili njama hizo amesema kuwa, maadui wamekosea katika mahesabu yao kwa kuwaunga mkono wafanyafujo na ghasia za hivi karibuni hapa nchini.