Oct 04, 2022 13:03 UTC
  • Bunge la Iran halikumpitisha Waziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii aliyependekezwa na Rais

Mohammad Hadi Zahedi Vafa, aliyependekezwa kuwa waziri wa Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii wa Iran, ameshindwa kupata kura ya kuwa na imani naye ya Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge).

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, wabunge wa bunge la Iran hawakupiga kura ya kuwa na imani na Mohammad Hadi Zahedivafa kushika nafasi ya Wizara ya Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii katika kikao cha leo cha bunge.

Kati ya kura zote 272 zilizohesabiwa za wabunge wote 274 waliokuwepo bungeni, wabunge 136 walipiga kura za "ndiyo", wabunge 125 walipiga kura za "hapana" na wabunge 9 waliamua kupiga kura ya kujizuia. Kwa matokeo hayo ni kwamba bunge halijakubaliana na kuteuliwa Zahedi Wafa kuwa waziri ya Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii.

Kwa mujibu wa kipengee cha "E" cha kifungu cha 117 cha kanuni za ndani za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, waziri anayependekezwa lazima apate wingi mutlaki wa kura za wabunge waliohudhuria kikao cha bunge. Kwa mujibu wa ibara hiyo, Zahedi Wafa alishindwa kupata kura moja ya ziada kumwezesha kuwa waziri wa wizara aliyopendekezwa.
Mohammad Hadi Zahedi Vafa

Kinyume na ilivyozoeleka katika nchi nyingi, ambapo Rais huwa na kauli ya mwisho katika kuteua baraza la mawaziri, katika mfumo wa utawala wa Iran unaotokana na ridhaa ya wananchi, mawaziri wanaopendekezwa na rais, huwajibika kwanza kwenda kujieleza bungeni, ikiwa na pamoja na kufafanua mipango yao ya utendaji kazi katika wizara husika. Hatimaye hupigiwa kura za kupitishwa au kukataliwa kushika nyadhifa walizopendekezewa na rais.

Vilevile, endapo utendaji wa waziri yeyote utakuwa si wa kuridhisha, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ina mamlaka ya kumwita kumsaili waziri huyo na ikiwa italazimu kumuuzulu kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.../