Oct 05, 2022 02:11 UTC

Iran imefanyia majaribio chombo kilichobuniwa na kutengenezwa nchini chenye uwezo wa kuhamisha satalaiti zilizo katika anga za mbali kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Chombo hicho kilichopewa jina la Saman na kutengenezwa na wataalamu na wahandisi kutoka Kituo cha Utafiti wa Anga cha Iran (ISRC), kilitumwa kwa mafanikio katika anga ya juu siku ya Jumanne na Wizara ya Ulinzi ya Iran.

"Kama sehemu ya juhudi za kupanua zaidi teknolojia ya mawasiliano ya ndani ya nchi na kutengeneza satalaiti inayozunguka kwenye eneo la anga za mbali linalojulikana kama obiti ya geostationary (GEO), uundwaji wa chombo hiki uliwekwa juu kwenye ajenda ya Kituo cha Utafiti wa Anga cha Iran," Hassan Salaryieh, kaimu mkuu wa wakala wa anga za juu wa Iran, alisema.

Ameongeza kuwa chombo hiki sasa kitaimarisha uwezo wa satalaiti za Iran kuzungua sayari ya dunia zikiwa katika anga za mbali zaidi na hivyo kuboresha utendaji kazi.

Amesema chombo hicho cha kuhamisha satalaiti kimeundwa kwa kutumi teknolojia nyeti na yenye gharama kubwa.

Chombo cha Saman cha kuhamisha satalaiti kilichoundwa Iran

 Mwezi Mei Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Issa Zarepour alisema, Iran ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazotengeneza na kurusha satalaiti katika anga za mbali na kusisitiza kuwa sekta hiyo inaipa Iran nguvu na teknolojia mpya.

Zarehpour alisema: Iran imepata maarifa na teknolojia ya hali ya juu zaidi katika uga wa anga za mbali katika kilele cha vikwazo na matatizo, kwa kadiri kwamba imefanikiwa kutengeneza satalaiti na maroketi ya kurushia satalaiti ambayo yanazifikisha satalaiti hizo katika maeneo yaliyokusudiwa angani kwa usahihi na umakinifu mkubwa.

Tofauti kubwa iliyopo kati ya mpango wa anga za juu wa Iran na nchi nyingine za eneo la Asia Magharibi ni kwamba Iran inategemea uwezo wake wa ndani na kunufaika na teknolojia yake ya asili bila kuwategemea wageni.