Oct 05, 2022 02:17 UTC
  • Nasser Kan'ani
    Nasser Kan'ani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali unafiki wa Marekani katika masuala ya haki za binadamu. Aidha amemtaka Rais Joe Biden wa Marekani ashughulikie rekodi mbaya ya haki za binadamu ya nchi yake na aondoe vikwazo vilivyo dhidi ya ubinadamu ilivyoiwekea Iran iwapo kweli anajali haki za binadamu.

Katika taarifa kupitia ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Ingekuwa bora iwapo kabla ya Joe Biden kuchukua misimamo ya haki za binadamu, kwanza  atafakari kuhusu rekodi ya haki za binadamu katika nchi yake, ingawa unafiki hauhitaji kutafakari."

Nasser Kan'ani ameongeza kuwa, Rais wa Marekani anapaswa kutafakari kuhusu vikwazo ambavyo Washington imeliwekea taifa la Iran kwani vikwazo hivyo ni mfano wa wazi wa jinai dhidi ya binadamu.

Ameongeza kuwa, watu kote duniani wanashuhudia taswira halisi ya haki za binadamu za Kimarekani katika nchi nyingi zikiwemo Palestina, Afghanistan, Iraq, Yemen, Libya, Syria na hata ndani ya Marekani kwenyewe.

Kan'ani ametoa kauli hiyo akijibu taarifa ya Ikulu ya White House Jumatatu ambapo Biden aliituhumu Iran kuwa eti imekandamiza kwa nguvu maandamano ya kitaifa kufuatia kifo cha mwamamke Muirani aliyefariki duniani hospitalini baada ya kuzimia katika kituo cha polisi mjini Tehran.

Rais Biden wa Marekani

Biden alisema, Marekani itaendelea kuunga mkono maandamano Iran ambayo yameandamana na ghasia za uharibifu wa mali ya umma. Waibua ghasia wametekeleza uharibifu mkubwa katika miji kadhaa huku wakiwashambulia maafisa wa usalama, kuharibu mali za umma na kuvunjia heshima matukufu ya kidini.

Akizungumza siku ya Jumatatu iliyopita mjini Tehran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisisitiza katika hafla ya pamoja ya wanachuo wahitimu wa Vyuo Vikuu vya vikosi vya ulinzi hapa nchini kwamba ghasia na machafuko yaliyoshuhudiwa hivi karibuni hapa nchini yaliratibiwa na Marekani na utawala ghasibu na bandia wa Israel na kusaidiwa kwa hali na mali na vibaraka wao na baadhi ya wasaliti raia wa Iran wanaoishi nje ya nchi.