Oct 05, 2022 12:58 UTC
  • Iran yamwita tena balozi wa Uingereza kulalamikia matamshi ya uingiliaji ya London

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemwita balozi wa Uingereza mjini Tehran, Simon Shercliff, kwa mara ya pili katika muda wa chini ya wiki mbili kutokana na uingiliaji wa London katika masuala ya ndani ya Iran.

Mkurugenzi Mkuu wa Ulaya Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema  leo Jumatano kwamba Tehran inapinga na kulaani vikali uingiliaji wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza katika masuala ya ndani ya Iran.

"Kwa bahati mbaya, kwa kutoa matamshi ya upande mmoja na ya kiupendeleo, upande wa Uingereza unaonyesha kuwa kweli una mkono katika njama za makundi ya adui yanayofanya kazi nchini humo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," amesema mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran.

Aidha  amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu itazingatia hatua inazoweza kuchukua katika kukabiliana na "hatua yoyote isiyo ya kawaida" ya upande wa Uingereza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema Jumatatu kuwa imemwita balozi mdogo wa Iran, mwanadiplomasia mkuu wa Iran nchini Uingereza hivi sasa, kuhusu kile ilichokiita ukandamizaji wa "kushtua" dhidi ya maandamano kufuatia kifo cha Mahsa Amini.

Afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema London inatumia "tafsiri za uwongo na za uchochezi" kuhusu matukio ya Iran ili kusogeza mbele mtazamo wake wa uingiliaji.

Maandamano yalizuka katika miji kadhaa Iran kufuatia kifo cha Amini, mwanamke wa Iran aliyekuwa na umri wa miaka 22 ambaye  alizirai katika kituo cha polisi mnamo Septemba 16 na siku kadhaa baadaye kutangazwa kuwa alifariki wakati akipata matibabu hospitalini.

Waibua ghasia wanaopata himaya ya madola ya kigeni kama vile Uingereza wamehusika katika kuharibu mali za umma nchini Iran

Iran imekuwa ikichunguza chanzo cha kifo cha msichana huyo, ikisema kuwa itachapisha ripoti mara tu itakapohitimisha uchunguzi huo.

Maandamano hayo, hata hivyo, yaligeuka kuwa ya vurugu na ghasia hivi karibuni, huku waandamanaji wanaoungwa mkono na madola ajinabi na yanayohasimiana na Iran wakivamia miji kadhaa na kuwashambulia maafisa wa usalama, sambamba na kutekeleza uharibifu dhidi ya mali za umma, na kuvunjia heshima matukufu ya kidini.

Mwishoni mwa Septemba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilimwita balozi wa Uingereza hapa nchini kuhusu "mazingira ya uadui" yaliyoundwa na vyombo vya habari vya lugha ya Kifarsi vilivyo London dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Siku ya Ijumaa Wizara ya Usalama ya Iran imesema Marekani na Uingereza zilichochea ghasia zilizoshuhudiwa hivi karibuni katika sehemu nyingi za nchi.