Oct 06, 2022 09:52 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Maadui wameungana kuvuruga usalama wa Iran ya Kiislamu

Naibu kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameashiria ghasia za hivi karibuni katika baadhi ya miji ya Iran na kusema kuwa katika fitna hiyo maadui wote waliingia uwanjani ili kuifanya Iran ya Kiislamu kutokuwa salama.

Kwa kisingizio cha kifo cha "Mahsa Amini", katika siku za hivi karibuni, waibua ghasia, kwa uchochezi wa vyombo vya habari vinavyopinga Mapinduzi ya Kiislamu walijitokeza katika baadhi ya miji ya Iran ambapo walitekeleza mauaji na kuharibu mali ya umma.

Ikumbukwe kuwa mwezi uliopita Mahsa Amini alielekezwa katika kituo cha polisi kwa ajili ya kupata mafunzo mafupi kuhusu vazi la Hijbu lakini akiwa hapo alizirai na kukimbizwa hospitalini lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia. Kifo cha binti huyo ambacho kiliwasikitisha wananchi na viongozi wa Iran kimetumiwa na maadui kuchochea fujo na ghasia katika baadhi ya miji ya Iran.

Kwa mujibu wa IRNA, Brigedia Jenerali Ali Fadavi, naibu kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi, akizungumza Alhamisi katika hafla ya kuwakumbuka mashahidi wa ghasia za Zahedan, amesema kwamba kwa zaidi ya miaka 43, vyombo vyote vya mfumo mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu vimekuwa vikichukua hatua ili adui asidhuru usalama wa taifa la Iran.

Waibua ghasia wanaopata himaya ya Marekani na waitifaki wake hivi karibuni waliibua fujo na kuharibu mali za umma Iran

Brigedia Jenerali Fadavi amefafanua kuwa, tangu siku ya kwanza ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, watawala wa madola ya kibeberu na kiistikbari wakiongozwa na Marekani wamekuwa wakitekeleza uadui dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema pamoja na kuwepo njama hizo, lakini mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran una mizizi imara.

Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu kuwa macho wananchi na mamlaka ya jeshi na vikosi vya usalama vya Iran ya Kiislamu na kuongeza kuwa maadui hadi sasa hawajafikia malengo yao yoyote machafu kuhusiana na kuvuruga usalama wa nchi.