Oct 07, 2022 07:54 UTC
  • Majasusi wawili wa Ufaransa wakiri majaribio ya kuchochea ghasia nchini Iran

Majasusi wawili wa Ufaransa waliokamatwa nchini Iran takriban miezi minne iliyopita wamekiri majaribio yao ya kuzusha maandamano na ghasia dhidi ya serikali kwa lengo kuu la kuweka shinikizo dhidi ya mfumo wa Kiislamu nchini.

Raia hao wawili wa Ufaransa, Cécile Kohler, 37, na Jacqeus Paris, 69, walisafiri Iran mnamo Aprili 28 kama watalii lakini ikabainika kuwa ni majasusi wa mashirika ya Magharibi.

Katika video iliyorushwa na kituo cha habari cha televisheni ya Iran cha al-Alam TV siku ya Alhamisi, Kohler alikiri kuwa jasusi wa Kurugenzi Kuu ya Usalama wa Nje ya Ufaransa (DGSE), ambayo ni sawa na mashirika ya kijasusi ya MI6 ya Uingereza na CIA ya Marekani.

Kohler amekiri kuwa yeye na mshirika wake walikuwa nchini Iran kwa lengo kuu la kuweka msingi wa machafuko makubwa katika jaribio la kuanzisha "mapinduzi" katika Jamhuri ya Kiislamu na kupindua serikali ya Iran.

Alieleza kwamba walileta kiasi kikubwa cha fedha ili kufadhili ghasia na migomo, na kununua silaha katika jaribio la kuzua fujo.

Kohler aliongeza kuwa silaha hizo zilikusudiwa kutumika "kupigana dhidi ya polisi," ikiwa italazimu. Kulingana na jasusi huyo mwingine, ambaye pia alionyeshwa kwenye video, lengo la DGSE lilikuwa "ni kuishinikiza serikali ya Irani."

Waibua ghasia Iran wanaopata himaya ya kigeni waliteketeza moto mali za umma 

Wizara ya Usalama ya  Iran ilitangaza mwezi Mei kwamba iliwakamata majasusi hao wawili wa Ufaransa baada ya kubainika kuwa walikuwa wanapanga njama za kuandaa na kuchochea ghasia na machafuko ya kijamii nchini Iran wakati wa maandamano ya walimu.

Kulingana na wizara hiyo, wawili hao walijaribu kuzua hali ya ukosefu wa utulivu na machafuko ya kijamii wakati baadhi ya walimu walipoingia barabarani katika maandamano ya amani ya kudai nyongeza ya mishahara na mazingira bora ya kazi.

Baadhi ya picha zinaonyesha kuwa wawili hao walihusishwa na wanaharakati wa vyama vya walimu akiwemo Rasoul Bodaghi.