May 27, 2017 13:37 UTC
  • Utawala wa Aal-Khalifa wapiga marufuku watu kushiriki mazishi ya watu uliowaua

Utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa nchini Bahrain umepiga marufu kujitokeza watu katika mazishi ya mashahidi waliouawa na askari wa utawala huo eneo la Dizar, kaskazini magharibi mwa mkoa wa Pwani wa nchi hiyo.

Kadhalika utawala huo umekataa kuikabidhi miili ya mashahidi hao waliouawa wakati wakimtetea Sheikh Isa Qassim, kiongozi mkuu wa Waislamu wa Shia nchi humo kwa familia zao sambamba na kuwapiga marufuku watu kushiriki katika marasimu hayo ya mazishi.

Ukandamizaji wa jeshi la Bahrain dhidi ya raia wa kawaida.

Wakati huo huo familia za mashahidi hao zimetoa taarifa zikisema kuwa, kituo cha polisi cha al-Haurah kimezipigia simu familia hizo na kusema kuwa ni watu wawili tu kutoka kila familia ndio watakaoshiriki mazishi hayo, kitendo ambacho kimetajwa kuwa ukandamizaji wa hali ya juu. Familia hizo zimesisitiza kuwa, kitendo cha utawala huo cha kuwazuia watu kushiriki katika mazishi hayo, kinahesabiwa kuwa ni jinai nyingine iliyotendwa na utawala huo. Kufuatia hali hiyo taasisi moja ya haki za binaadamu nchini Bahrain imetangaza kuwa, watawala wa nchi hiyo wanajaribu kufunika jinai walizozifanya eneo la Diraz na kwamba, wana wasi wasi mkubwa wa ushiriki wa watu katika mazishi hayo.

Sheikh Isa Qassim, alimu mkubwa wa nchini Bahrain

Jumapili iliyopita, utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa ulitoa hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja dhidi ya Sheikh Isa Qassim sambamba na kutaifisha mali zake, huku askari wa utawala huo wakivamia eneo la Diraz siku ya Jumanne iliyopita yakiwamo makazi ya alimu huyo mkubwa. Katika hujuma hiyo askari hao waliwaua watu sita na kujeruhi zaidi ya wengine 200 na kuwatia mbaroni karibu watu 300.

 

Tags