Jun 11, 2018 02:41 UTC
  • Tangazo la Taliban la kusitisha vita na kupokewa vyema na serikali ya Afghanistan

Serikali ya Afghanistan imetangaza kulikaribisha kwa mikono miwili tangazo lililotolewa na kundi la Taliban la kusitisha vita katika siku za Idul-Fitri.

Shah Hussein Mortazavi, Naibu Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Afghanistan amelitaja tangazo la usitishaji vita la kundi la Taliban, kuwa ni mwanzo mzuri na kwamba serikali ya Kabul inatarajia kutumia usitishaji vita huo kuimarisha usalama na amani nchini humo. Aidha ameonyesha matumaini  yake kwamba, kundi la Taliban na kupitia ombi la maulamaa wa kidini na wananchi, litatoa jibu chanya na kuhitimisha kabisa vita ndani ya nchi hiyo ya barani Asia. Jumamosi iliyopita kundi la Taliban lilitoa taarifa na kutangaza kwamba, litasitisha mapigano katika siku zote za Idul-Fitr kwa kuacha kuwashambulia askari wa serikali lakini likaongeza kwamba, wapiganaji wake hawatositisha mashambulizi dhidi ya askari wa kigeni na kwamba mashambulizi yake yataendelea dhidi ya askari hao vamizi kama kawaida.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan

Lengo la hatua hiyo ya genge la Taliban katika maamuzi hayo, ni kuandaa anga nzuri ya kuwaruhusu wananchi kujuliana hali katika siku za idi. Aidha hatua hiyo imejiri baada ya Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan na Baraza la Maulamaa la nchi hiyo kutoa pendekezo la kuheshimiwa mwezi huu wa Ramadhan sambamba na kusitisha vita vya pande mbili. Hata hivyo pendekezo la Rais Ghani kwa kundi la kigaidi la Taliban kuhusu kusitisha mapigano lilianza tangu mwanzoni mwa mwezi huu mtukufu, na baada ya kundi hilo kupuuza pendekezo hilo, rais huyo aliamua kutangaza usitishaji vita wa upande mmoja kuanzia tarehe 27 mwezi huu yaani tarehe 12 Juni hadi siku tano za baada ya sherehe za Idul-Fitr.

Shah Hussein Mortazavi, Naibu Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Afghanistan

Radiamali ya kundi la Taliban kwa pendekezo la Baraza la Maulama la Afghanistan sambamba na tangazo la usitishaji vita la upande mmoja la Rais Ashraf Ghani kupitia usitishaji wa siku tatu kwa mnasaba wa Iddil-Fitri, inaonyesha kwamba hivi sasa genge hilo linakabiliwa na mashinikizo ya walio wengi na vyombo vya habari kiasi cha kulifanya likubali pendekezo hilo la serikali ya Kabul. Hata kama kundi hilo linadai kuwa uamuzi wake huo una lengo la kuandaa mazingira ya kuwawezesha wananchi kutekeleza ibada za mwezi wa Ramadhan ikiwemo swala ya iddi na pia kuwaruhusu wananchi hao kujuliana hali, lakini sisitizo la genge hilo la kuendeleza mashambulizi dhidi ya askari wa kigeni huko Afghanistan, linakinzana na malengo hayo. Kwa mujibu wa tangazo la kundi hilo, wapiganaji wake wataendeleza mashambulizi katika kipindi chote cha usitishaji vita wa hivi sasa dhidi ya askari wa Marekani na wale wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO), hivyo mapigano na utumiaji nguvu vitakavyosababishwa na mashambulizi hayo vitazidi kuuweka matatani usalama wa wananchi suala ambalo kimsingi linazusha maswali mengi kuhusiana na ukweli wa tangazo hilo la usitishaji vita.

Rais wa Afghanistan ambao daima wamekuwa wahanga wa mashambulizi ya genge la Taleban

Inafaa kuashiria kuwa, kwa mara kadhaa kundi hilo limewahi kudai kwamba katika vita vyake nchini Afghanistan lengo lake kuu si wananchi, lakini ukweli uliopo unaonyesha kwamba sehemu kubwa ya hujuma zake zinawalenga wananchi na hivyo kuthhibitisha kwamba vitendo vya genge hilo ni hatari kubwa dhidi ya raia wa kawaida wa Afghanistan. Mtazamo huo unapata nguvu kupitia tangaza la kundi hilo la kuwaondoa askari wa Marekani na NATO katika mchakato wa usitishaji vita ambapo kwa mujibu wa weledi wa mambo, hatua hiyo inakusudia kuchochea fikra za walio wengi sambamba na kuiweka serikali ya Kabul katika mashinikizo ya wananchi walio na hamu kubwa ya kuonda serikali ya nchi yao inawatimua askari hao wa kigeni ndani ya nchi hiyo.

Askari vamizi wa Marekani

Hata hivyo kwa kuzingatia radiamali ya kundi hilo, nadharia hii inapata nguvu kwamba, hata baada ya askari wa Marekani na NATO kuondoka nchini humo, wanachama wa Taliban hawatositisha vitendo vya utumiaji mabavu na mashambulizi yao kuwalenga wananchi. Kadhalika kundi hilo litaendeleza vita nchini Afghanistan kupitia ajenda yake ya kile linachodai kuwa ni kusimamisha Uislamu unaofuata idolojia ya Uwahabi na ambao kimsingi unatofautiana na mafundisho asili ya Uislamu ulioletwa na Mtume Muhammad (saw). Kwa mantiki hiyo tunaweza kusema kuwa, tangazo la Taliban la kusimamisha vita dhidi ya skari wa serikali tu, halina maana kwa kuwa bado usalama na amani vitaendelea kuwa matatani kupitia mashambulizi ya kile kinachotajwa kuwa ni vita dhidi ya askari wa NATO na Marekani.

Tags

Maoni