Jun 20, 2018 07:31 UTC
  • Wasiwasi wa UN juu ya maafa ya kibinadamu katika mji wa Al Hudaydah nchini Yemen

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa watu 26,000 wakazi wa mji wa bandari wa Al-Hudaydah magharibi mwa Yemen wamelazimika kuzihama nyumba na makazi yao baada ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kushambulia eneo hilo.

Stephane Dujarric ameongeza kuwa kutokana na kuendelea kwa mapigano mjini Al Hudaydah idadi ya wakimbizi hao inatazamiwa kuongezeka.

Mnamo mwezi Machi mwaka 2015, Saudi Arabia, ikiungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya waitifaki wake wengine iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa ardhini, baharini na angani. Moto wa vita uliowashwa na Saudia, Imarati na waitifaki wao, hadi sasa umesha sababisha vifo vya Wayemeni zaidi 14,000, makumi ya maelfu kujeruhiwa na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Wakazi wa mji wa Al Hudaydah wakilazimika kuyahama makazi yao

Kwa upande mwingine, na kwa lengo la kufidia kushindwa kwake katika kufikia malengo yake, muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia Jumatano iliyopita ya tarehe 13 Juni ulishadidisha mashambulio na hujuma za kijeshi dhidi ya bandari ya Al Hudaydah kwa kisingizio eti bandari hiyo inatumiwa kuingiza kimagendo silaha na zana za kivita nchini Yemen. Bandari ya Al Hudaydah ndio njia kuu ya kupitishia misaada ya kibinadamu inayotumwa kwa ajili ya wananchi madhulumu na wanaoatilika kwa vita wa Yemen. Utawala vamizi wa Aal Saud na waitifaki wake wanafanya juu chini ili kuhakikisha kuwa, kwa kuidhibiti bandari hiyo na kuzuia misaada ya kibinadamu isiingizwe nchini Yemen waweze kushadidisha mashinikizo yao dhidi ya harakati ya muqawama ya wananchi na kupata njia ya kuiweka nchi hiyo chini ya mamlaka yao.

Mandhari ya bandari ya Al-Hudaydah kabla ya hujuma za kijeshi za Saudia na waitifaki wake

Mashambulio ya kila upande dhidi ya bandari ya Al Hudaydah yalianzishwa na yangali yanaendelezwa katika hali ambayo hali ya kibinadamu nchini Yemen ni mbaya sana, huku uhaba mkubwa wa bidhaa za chakula na dawa ukiwa unatishia na kuhatarisha maisha ya maelfu ya raia wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti za asasi za kimataifa, Wayemeni milioni 22 wanahitajia msaada huku milioni nane kati yao wakiwa wanakabiliwa na baa la njaa na ukame.

Lise Grande, mratibu wa UN wa masuala ya kibinadamu Yemen

Lise Grande, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu nchini Yemen anaizungumzia hali hiyo kwa kutoa indhari kwamba: Hujuma na mashambulio dhidi ya Al Hudaydah yanaweza kugharimu maisha ya watu laki mbili na nusu.

Saudi Arabia ikishirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati zinashadidisha hujuma na mashambulio yao dhidi ya mji wa bandari wa Al Hudaydah katika hali ambayo, Marekani na Uingereza, zinazojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu ni waungaji mkono wakuu wa jinai zinazofanywa na tawala hizo mbili za Kiarabu dhidi ya taifa masikini la Yemen.

Maafa ya kibinadamu ya Yemen yanayosababishwa na Saudia kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani

Bernie Sanders, Seneta wa jimbo la Vermont nchini Marekani anasema, ushrikiano inaotoa Marekani kwa utawala wa Saudi Arabia unachangia kuendelea na kushadidi hali mbaya ya kibinadamu nchini Yemen; na anasisitiza kwa kusema: Serikali ya Marekani inapaswa kukomesha ushiriki wake haramu na usio na kibali cha kisheria katika vita vya Yemen.

Alaa kulli hal, utawala wa Saudia na waitifaki wake hadi sasa wameshindwa kufikia malengo yao nchini Yemen kutokana na muqawama na kusimama imara wananchi wa nchi hiyo. Na kwa sababu hiyo, Aal Saud na washirika wake wa Magharibi na wa Kiarabu wanahisi njia pekee ya kufanya ni kushadidisha operesheni na hujuma za kijeshi dhidi ya njia pekee ya mawasiliano ya Wayemeni na ulimwengu wa nje ili kwa kuwadhikisha na kuwatesa kwa njaa wananchi hao, waweze kupunguza joto la kinyongo walichonacho kwa kushindwa kufikia malengo yao nchini Yemen. Lakini sambamba na hayo matarajio ya walimwengu ni kuziona jumuiya za kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa ukichukua hatua za kivitendo badala ya kutosheka na kutoa taarifa za maneno matupu ili kuzuia kuendelea maafa makubwa zaidi ya kibinadamu yanayoshuhudiwa duniani.../

 

Tags