Aug 08, 2018 04:13 UTC
  • Marekani, Saudia zashirikiana na Al Qaeda Yemen kukabiliana na Ansarullah

Uchunguzi mpya umebaini kuwa muungano unaoongozwa na Saudia katika vita dhidi ya watu wa Yemen unashirikiana na magaidi wa Al Qaeda chini ya maelekezo ya Marekani kwa lengo la kukabiliana na harakati ya Ansarullah.

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Associated Press unaonyesha kuwa Saudia ilifikia mapatano ya siri na Al Qaeda kwa lengo la kutoa mafunzo kwa magaidi wakufurishaji ili watekeleze opareseni dhidi ya harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah.

Taarifa hiyo imepelekea kutiliwa shaka madai ya hivi karibuni ya muungano unaaongozwa na Saudia ambao umekuwa ukidai kupata ushindi dhidi ya magaidi wa Al Qaeda. Aidha taarifa hiyo imeweka wazi ukweli kuwa, Marekani, Saudi Arabia na waitifaki wao nchini Yemen wamekuwa wakishirikiana na magadii wa Al Qaeda.

Uchunguzi umebaini kuwa muungano unaoongozwa na Saudia umewaajiri mamia ya magaidi wa Al  Qaeda na kwamba Marekani imeafiki jambo hilo.

Wapiganaji wa Ansarullah

Uchunguzi huo umetegemea ripoti na mahojiano na maafisa wa Yemen wakiwemo maafisa wa usalama na kijeshi, wapatanishi wa kikabila na magaidi wa al Qaeda.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani harakati ya Ansarullah na kumrejesha katika utawala Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia.

Tags