Aug 31, 2018 06:32 UTC
  • Qatar yazishutumu Saudia, UAE kwa kushirikiana na magaidi wa al Qaeda nchini Yemen

Balozi wa Qatar nchini Marekani amezishutumu Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuwa na ushirikiano wa siri na magaidi wa al-Qaeda nchini Yemen.

Katika makala aliyochapisha katika gazeti la Washington Post, Sheikh Meshal bin Hamad Aal Thani, balozi wa Qatar nchini Marekani amesema, Saudia na UAE zinahatarisha usalama wa eneo hili zima kwa kuwawezesha magaidi wakufurishaji wa al-Qaeda kuendesha kwa uhuru harakati zao nchini Yemen.

Balozi huyo wa Qatar ameongeza kuwa,  badala ya Saudia na UAE kuchukua hatua za kurejesha amani na kukomesha maafa ya kibinadamu ambayo yanazidi kuongezeka nchini Yemen,  (nchi hizo mbili) zinashirikiana na magaidi wa al-Qaeda.

Mwandiplomasia huyo wa Qatar ametoa kauli hiyo kufuatia uchunguzi wa Shirika la Habari la Associated Press ambao hivi karibuni umefichua kuwa, muungano wa kijeshi unaaongozwa na Saudia katika vita dhidi ya Yemen unashirikiana na magaidi wa al-Qaeda nchini humo.

Sheikh Meshal bin Hamad Al Thani, Balozi wa Qatar nchini Marekani

Aidha Balozi Meshal amesema Saudia na UAE zina historia ndefu ya kuunga mkono magaidi na kusema kuwa, sera hiyo imekuwa na matokeo mabaya kwani imepelekea kuenea ugaidi na mfano wa wazi ni hujuma za kigaidi zilizotokea nchini Marekani mwezi Septemba 2001 na hujuma dhidi ya balozi za Marekani huko Kenya na Tanzania. Amesema karibu wahusika wote wa hujuma za Septemba 11 walikuwa ni raia wa Saudia na UAE.

Matamshi hayo ya balozi wa Qatar yamekuja huku mgogoro ukiendelea kutokota baina ya nchi hiyo na madola manne ya Kiarabu yaani  Saudia, UAE, Bahrain na Misri huku kiranja wao ikiwa ni Saudi Arabia.

Tags