Dec 16, 2018 07:34 UTC
  • Al Houthi: Tarehe ya kusimamishwa vita al Hudaydah Yemen imeshajulikana

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amesema kuwa, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen ameukabidhi ujumbe wa San'a unaoshiriki kwenye mazungumzo ya amani ya nchi hiyo huko Sweden, tarehe ya kusimamisha vita katika mkoa wa al Hudaydah.

Mohammad Ali al Houthi amesema hayo usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa, Martin Griffiths, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika suala la Yemen ameshaainisha siku ya kusimamisha vita al Hudaydah, hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu siku hiyo.

Kwa upande wake, Salim al-Moughaless, mjumbe wa timu ya mazungumzo ya Answarullah ameutaka Umoja wa Mataifa na jamii ya Kimataifa kuishinikiza Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kuheshimu vipengee vya makubaliano ya amani. Ameongeza kuwa, matukio ya al Hudaydah yanathibitisha kuwa muungano wa Saudi Arabia hauheshimu mapatano ya amani.

Martin Griffiths, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika suala la Yemen

 

Kwa mujibu wa Yahya Sarii, msemaji wa majeshi ya Yemen, muungano wa Saudi Arabia umefanya mashambulizi 21 ya anga na ya mizinga katika kipindi cha masaa 24 ya tangu kumalizika mazungumzo ya Sweden katika fukwe za magharibi za mkoa wa al Hudaydah.

Jana pia, muungano huo vamizi wa Saudi Arabia ulishambulia kwa risasi 15 za mizinga eneo la "Julai 7" huko Yemen.

Duru ya nne ya mazungumzo ya Yemen ilifanyika siku ya Alkhamisi ya tarehe 6 Disemba mjini Stockholm Sweden chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa na pande mbili zimefikia makubaliano ya kusimamisha vita katika baadhi ya maeneo ya Yemen ukiwemo mji wa bandari wa al Hudaydah.

Tags

Maoni