Jan 09, 2019 07:03 UTC
  • Ansarullah: Hakuna hatua iliyochukuliwa kwa ajili ya kusitisha mapigano al Hudaydah

Afisa Uhusiano wa Nje wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, hakuna hatua yoyote ya kivitendo iliyochukuliwa kwa ajili ya kutekeleza mapatano ya kusitisha mapigano katika mji wa bandari wa al Hudaydah magharibi mwa Yemen na kubadlishana mateka kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa mjini Stockholm, Sweden.

Adnan Qassim Ali Qasim Ali amemtaka Martin Griffiths, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen achukue hatua za kuhakikisha kwamba usitishaji vita unadumishwa huko al Hudaydah na kuongeza kuwa, Wayemeni milioni 27 wanahitaji misaada ya kibinadamu na wengine zaidi ya milioni nne wamepoteza makazi yao. 

Afisa huyo wa harakati ya Ansarullah ameashiria pia hali mbaya waliyonayo wananchi wa Yemen kutokana na mashambulizi ya kidhalimu yanayoendelea kufanywa na utawala wa Saudi Arabia na washirika wake na kueleza kuwa, mashambulizi yasiyo ya kawaida ya utawala wa Aal Saud yamewasababishia wananchi wa Yemen magonjwa kama dondakoo na kipindupindu.

Watoto wadogo ni miongoni mwa raia wa Yemen wanaotabika na maradhi ya kipindupindu 

Duru ya nne ya mazungumzo ya amani ilifanyika Disemba 6 mwaka jana mjini Stockholm Sweden na kuendelea kwa muda wa wiki moja. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na makundi mbalimbali ya Yemen na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen ambapo pande husika zilisaini makubaliano ya kusitisha mapigano na uhasama katika mji wa bandari wa al Hudaydah huko magharibi mwa Yemen.   

Tags

Maoni