Feb 05, 2019 13:11 UTC
  • Uungaji mkono wa kila upande wa Marekani na Saudi Arabia kwa kundi la al-Qaeda

Kanali ya televisheni ya CCN imetangaza katika ripoti yake kwamba, Saudi Arabia imekuwa ikilipatia kundi la kigaidi la al-Qaeda silaha ambazo Marekani imeupatia muungano wa Kiarabu katika vita dhidi ya Yemen.

Serikali ya Washington mbali na kuupatia utawala wa Aal Saud silaha  nyingi imekuwa ikizitilia mafuta ndege za kijeshi za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen. Aidha Marekani imekuwa ikitathmini taarifa za operesheni za kijeshi katika vita dhidi yay Yemen, kusimamia na kuongoza vita hivyo.

Kwa hakika Marekani inahesabiwa kuwa muungaji mkono wa kwanza na mhalalishaji wa vita vya kidhalimu dhidi ya Yemen na Washington imelionyesha wazi hili katika hatua yake ya kuiuzia Saudia silaha zenye thamani ya dola bilioni 500 katika fremu ya mkataba wa "Muamala wa Karne."

Wanachama wa kundi la al-Qaeda

Kufichuliwa zaidi duru mpya ya hatua za Marekani na Saudi Arabia za kuyaunga mkono makundi ya kigaidi kunazidi kudhihirisha kuweko uratibu wa kijeshi wenye njama nyuma ya pazia ya Riyadh na Washington. Ushirikiano wa Marekani na Saudi Arabian katika kuwapatia silaha magaidi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Yemen haujaanza leo wala jana.

Takribani miaka miwili iliyopita, duru za Yemen zilitangaza kuwa, Saudi Arabia imewaingiza nchini Yemen mamluki 400 wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh. Magaidi hao waliingizwa na Saudia katika Bandari ya Aden kusini mwa Yemen kwa meli ndogo wakitokea Syria ili watumwe katika medani za vita katika pwani ya magharibi mwa Yemen.

Hii ni katika hali ambayo, sambamba na hatua hiyo, ndege nne za Marekani zenye uwezo wa kubeba ndege za kijeshi zilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden zikiwa na kiwango kikubwa cha silaha na zana za kijeshi. Kwa maneno mengine ni kuwa, Saudi Arabia iliwatoa wanachama wa makundi ya kigaidi huko nchini Syria  na maeneo mengine na kuwapeleka nchini Yemen, huku Marekani ikiwa na jukumu la kuwapatia silaha na zana za kivita magaidi hao.

Wapiganaji wa al-Qaeda nchini Yemen

Kwa hakika hili ni jambo ambalo limeweka wazi wigo mwingine wa himaya na uungaji mkono wa kila upande wa Marekani na Saudi Arabia kwa makundi ya kigaidi. Ushirikiano wa Saudi Arabia na madola ya Magharibi katika kuwaunga mkono magaidi haujawa na natija nyingine bighairi ya kushadidisha vitendo vya kikatili kieneo na kimataifa.

Saudi Arabia imeendelea kuzatitiwa kwa silaha za madola ya Magharibi katika hali ambayo, hatua za utawala huo zimekuwa zikikinzana dhahir shahir na  amani na usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia.

Nyaraka na ushahidi wa kutegemewa unaonyesha juu ya kuweko nafasi na mchango wa siri na wa dhahiri wa Saudia Arabia katika kuyapatia silaha makundi ya kitakfiri ambayo chimbuuko lake ni mafundisho ya Kiwahabi.

Katika upande wa pili, Marekani nayo imeendelea na siasa zake za kuwahadaa walimwengu kwamba, eti inapambana na makundi ya kigaidi likiwemo la al-Qaeda. Kwa hakika, Marekani imekuwa ikitumia visingizio mbalimbali na hivyo kukiuka mara kwa mara mamlaka ya kujitawala Yemen.

Mfalme wa Saudi Arabia akitilia saini mkataba na Rais Donald Trump wa Marekani

Katika miezi ya hivi karibuni kila mara kumekuwa kukiripotiwa habari kwamba, idadi kadhaa ya wanajeshi wa Marekani wameingia nchini Yemen kwa kisingizio cha kwenda kupambana na wanachama wa kundi la kigaidi la al-Qaeda ambapo hilo linabainisha kuweko harakati za kutiliwa shaka za Marekani katika eneo ikishirikiana na utawala wa kifalme wa Aal Saud. Makundi ya kigaidi ya Daesh, al-Qaeda na Taliban chimbuko lao ni fikra za Kiwahabi za Saudia.

Saudi Arabia ikiwa muenezaji wa fikra za Kiwahabi na Kisalafi, imekuwa chimbuko la kulea na kueneza ugaidi katika maeneo mbalimbali ya dunia. Katika mazingira kama haya, serikali ya Washington kutokana na kushirikiana na Riyadh na katika fremu ya siasa za kutanguliza mbele maslahi yake sambamba na kunufaika zaidi na harakati za makundi ya kigaidi katika njia yake ya kufikia malengo yake ya kuzusha fitina imelifanya suala la kusimamia na kueneza makundi na fikra za kigaidi  kuwa miongoni mwa ajenda zake.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu, uchupaji mipaka na ukosefu wa usalama duniani, ni matunda ya siasa za Saudi Arabia za kueneza fikra za Uwahabi kwa uungaji mkono wa kila upande wa serikali ya Marekani.

Tags