Mar 12, 2019 02:54 UTC
  • Spika wa Bunge la Lebanon: Eneo lote la Quds ni mji mkuu wa Palestina

Spika wa Bunge la Lebanon kwa mara nyingine tena amesisitiza msimamo wa nchi yake kuhusiana na kuiunga mkono Baytul -Muqaddas na Palestina na kusema kuwa, eneo lote la Quds Tukufu ni mji mkuu wa nchi ya Palestina.

Nabih Berri amesema hayo Beirut mji mkuu wa Lebanon alipokutana na ujumbe wa Taasisi ya Kimataifa ya Quds na kusema bayana kwamba, Quds ni chimbuko la umoja na mshikamano wa Waislamu na kwamba, Waislamu wanapaswa kufanya hima na juhudi kuulind mji huo mtakatifu.

Spika wa Bunge la Lebanon amesema kuwa, Waislamu wanapaswa kusimama na kuulinda mji wa Beitul-Muqaddas mbele ya njama za kila leo za utawala vamizi wa Israel.

Nabih Berri  amesisitiza kuwa, msimamo wa Lebanon ni kukombolewa kikamilifu Palestina kwa kutumia nyenzo, mbinu na mikakati yote inayowezekana kutumiwa.

Spika wa Bunge la Lebanon ameashiria mkutano wa Jumuiya ya Mabunge ya Kiarabu uliofanyika mwanzoni mwa mwezi huu kuhusiana na Quds na kusema kuwa, mahudhurio makubwa ya Maspika wa Mabunge ya Kiarabu katika mkutano huo ilikuwa ishara tosha kwamba, mji wa Beitul Muqaddas ungali una nafasi maalumu katika umma wa Kiarabu na Kiislamu.

Mji wa Quds

Nabih Berri ameonya kuhusiana na juhuudi na mikakati ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Juhudi za kuanzisha uhusiano na kawaida na Israel za baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo hili la Magharibi ya Asia hususan Saudi Arabia na Imarati zimeonekana zikishika kasi katika miezi ya hivi karibuni. Juhudi hizo zinafanyika katika hali ambayo, kwa miaka mingi sasa Israel mbali na kuwakandamiza Wapalestina imeyakalia kwa mabavu maeneo mengi ya Kiislamu na Kiarabu.

Tags