May 06, 2019 13:32 UTC
  • Utawala wa Kizayuni umelazimika kukubali usitishaji vita kati yake na Palestina

Duru za habari za Palestina zimetangaza kuwa utawala wa Kizayuni hatimaye umekubali kusimamisha vita ulivyovianzisha huko Ukanda wa Ghaza kutokana na mashinikizo ya fikra za walimwengu kutoka nchi mbalimbali duniani.

Makubaliano hayo ya kusimamisha vita kati ya makundi ya muqawama ya Palestina na jeshi la utawala wa Kizayuni yamefikiwa mjini Cairo kufuatia juhudi za Umoja wa Mataifa na Misri. Makubaliano hayo yameanza kutekelezwa leo asubuhi. 

Masaa kadhaa kabla ya kutangazwa usitishaji vita huo, duru za habari za Palestina zilitangaza kuwa makundi ya muqawama ya Palestina hayajaafiki mpango wa kusimamisha mapigano na Israel; na kwamba jumbe za Hamas na Jihadul Islami ambazo zimeelekea Cairo zinasisitiza kuwa makubaliano ya kusimamisha vita ya huko nyuma yanapasa kutekelezwa na utawala wa Tel Aviv bila ya masharti yoyote. Utawala wa Kizayuni umeamua kufikia makubaliano ya kusimamisha mapigano na makundi ya muqawama baada ya kuuliwa watu watano na kujeruhiwa wengine zaidi ya mia moja katika upande wa utawala wa Kizayuni katika mashambulio ya makombora ya wanamuqawama dhidi ya mashambulizi ya kikatili ya jeshi la Kizayuni huko Ghaza na baada ya kuuliwa raia wa Palestina. 

Mtoto wa miezi 14 aliyeuliwa shahidi katika mashambulizi ya Israel huko Ghaza 
 

Utawala wa Israel umetangaza kuwa siku mbili zilizopita makombora 600 yamevurumishwa kuelekea katika vitongoji vya Kizayuni yakitokea Ukanda wa Ghaza. Wizara ya Afya ya Palestina pia imetangaza kuwa Wapalestina 25 wameuawa shahidi na 170 kujeruhiwa katika mapigano ya siku mbili zilizopita kati ya makundi ya wanamuqawama na jeshi la utawala wa Kizayuni. 

Tags

Maoni