May 22, 2019 07:51 UTC
  • Saudia kuwanyonga wanazuoni 3 mashuhuri baada ya Ramadhani

Utawala wa Aal-Saud umepanga kuwanyonga wanazuoni watatu mashuhuri nchini Saudi Arabia baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ikiwa ni katika muendelezo wa ukatili na ukandamizaji dhidi ya wasomi na wapinzani unaoongozwa na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa utawala huo, Mohammed bin Salman.

Tovuti ya habari ya Middle East Eye yenye makao makuu yake mjini London imeripoti kuwa, watawala wa Riyadh wamepanga kuwanyonga wanazuoni hao mashuhuri ambao ni Sheikh Salman al-Ouda, Sheikh Awad al-Qarni na Ali al-Omari kwa tuhuma bandia za ugaidi.

Sheikh Ouda ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu, ambayo Riyadh imeiweka katika orodha yake ya mashirika ya kigaidi. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanamfahamu mwanazuoni huyo kama mwanamageuzi.

Sheikh al-Qarni pia ni mwanachuoni mashuhuri nchini Saudia, mwanaakademia na mwandishi mtajika, huku al-Omari akifahamika zaidi kuwa mtangazaji mashuhuri wa Kiislamu.

Mwezi uliopita, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia ilitangaza kuwa imewaua watu 37 raia wa nchi hiyo ambapo 32 kati yao ni Waislamu wa Kishia kwa tuhuma za kile kilichotajwa na wizara hiyo kuwa ni ugaidi.

Chinja chinja ya Saudia

Kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar imenukuu duru za habari ndani ya utawala wa Aal-Saud zikisema kuwa, kitendo hicho cha Riyadh kuwanyonga kwa umati Waislamu wa madhehebu ya Shia kilikusudia kupima kiwango cha lalama za jamii ya kimataifa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International mwaka jana, utawala wa Aal Saudi uliwaua watu 149 kwa tuhuma hizo hizo za ugaidi.

Tags