Jun 21, 2019 07:10 UTC
  • Malengo na umuhimu wa safari ya Amir wa Kuwait nchini Iraq

Swabah al-Ahmad al-Jabir as-Swabah Amir wa Kuwait siku ya Jumatano alifanya safari nchini Iraq ambapo alilakiwa na kufanya mazungumzo na Rais Barham Swaleh wa nchini hiyo.

Kuzungumzia uhusiano wa pande mbili na masuala ya kieneo ni lengo muhimu la safari ya Amir as-Swabah nchini Iraq. Uhusiano wa nchi mbili hizi umekuwa ukiimarika katika miaka ya hivi karibuni. Moja ya dalili za hamu ya nchi hizo kuimarisha uhusiano wao ni kutembeleana viongozi wa nchi hizi jirani. Safari hizo zimekuwa zikifanyika katika ngazi za juu kidiplomasia.

Adil Abdul Mahdi Waziri Mkuu wa Iraqi aliitembelea Kuwait tarehe 22 Mei mwaka huu baada ya Rais Barham Swaleh wa Iraq kuitembelea mwezi Novemba mwaka jana 2018, muda mfupi baada ya kuapishwa kuwa rais wa nchi hiyo. Hivi sasa Amir wa Kuwait amefanya safari yake ya pili huko Iraq baada ya kuapishwa kuwa Amir wa Kuwait. Alifanya safari yake ya kwanza huko Iraq mwaka 2012 kwa lengo la kushiriki kikao cha wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilichofanyika mjini Baghdad. Malengo ya safari hizo yamekuwa ni kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pia kuondoa mivutano inayoharibu uhusiano huo. Kuhusiana na suala hilo, Khalid al-Jarullah, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait ameisifu safari ya hivi karibuni ya Amir wa Kuwait huko Baghdad kuwa ni ya kihistoria na kuongeza kuwa imefanyika katika kivuli cha uhusiano wa kidugu uliopo baina ya nchi hizo. Amir wa Kuwait pia amesema kuwa nchi yake ina nia ya kuisaidia Iraq kupambana  na makundi ya kigaidi na katika ukarabati wa nchi hiyo.

Amir wa Kuwait akilakiwa nchini Iraq

Safari ya Amir wa Kuwait nchini Iraq pia ina umuhimu mkubwa katika mtazamo wa kieneo. Safari hiyo imefanyika katika hali ambayo eneo la Asia Magharibi linashuhudia mvutano ambao haujawahi kushuhudiwa kwa miaka mingi. Mvutano huo unajiri kati ya madola makubwa ya kieneo na pia kati ya nchi za Kiarabu.

Mvutano mwingine unaendelea kuongezeka kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani. Wakati huohuo vitendo vya uharibifu na kushambuliwa meli za kubebea mafuta vinavyofanywa na pande zisizojulikana vinaendelea kushuhudiwa. Jinai zinazotekelezwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na watawala wa Saudia dhidi ya taifa la Yemen, jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina na mpango hatari wa Mualama wa Karne ni mambo yanayoendelea kufuatiliwa na maadui kwa madhara ya mataifa ya Asia Magharibi (Mashariki ya Kati). Katika mazingira hayo ambapo nchi kama vile Saudia na Imarati zinatekeleza njama za kuibua tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa madhumuni ya kuzidisha mvutano kati yake na Marekani, nchi kama Kuwait na Iraq zinafuatilia sera za kupunguza mvutano katika eneo hili.

Rais Barham Salih wa Iraq akiwa katika kikao cha wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Makka

Amir wa Kuwait daima amekuwa akifuatilia siasa za kupunguza mvutano kati ya nchi za Mashariki ya Kati zikiwemo juhudi zake za kupunguza mvutano kati ya Iran na Saudia, Qatar na Saudia na vilevile kati ya Iran na Marekani. Katika umri wake wa miezi minane pekee, serikali ya Baghdad pia imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuimarisha usalama na kujitawala kisiasa eneo hili muhimu duniani. Nchi hiyo pia imekuwa ikifanya juhudi za kupunguza mvutano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudia na kati ya Iran na Marekani. Katika kutekeleza siasa zake huru za nje serikali ya Baghdad si tu kwamba inajiepusha kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya nchi nyingine bali imekuwa ikipinga vikali siasa za nchi tofauti kutoa tuhuma kama hizo dhidi ya nchi nyingine. Mfano wa jambo hilo ulionekana wazi kupitia hotuba ya Rais Barham Swaleh katika kikao cha 30 cha wakuu wa nhi za Kiarabu huko Makka katika kujibu tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa na mfalme wa Saudia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na badala yake kuashiria siasa imara za Iran katika kuimarisha amani na usalama wa eneo kama stratijia muhimu ya siasa zake za kieneo.

Tags