Sep 10, 2019 07:17 UTC
  • Nasrullah: Hizbullah na Iran haziwezi kuyumbishwa na mashinikizo

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema harakati hiyo ya muqawama na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zitaendelea kusimama kidete dhidi ya mashinikizo na vikwazo vya Marekani.

Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo usiku wa kuamkia leo katika hotuba fupi aliyoitoa kwa mnasaba wa usiku wa kuamkia Siku ya Ashura ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS katika jangwa la Karbala nchini Iraq.

Amebainisha kuwa, "Tunapigana vita vikubwa, Marekani na utawala haramu wa Israel zinajaribu kuzingira kambi yetu ili zitupigishe magoti lakini hilo haliwezi kufua dafu."

Sayyid Nasrullah ameleza bayana kuwa, "Hii leo, kiongozi wa kambi yetu ni Imam Khamenei (Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu), ambapo Marekani inafanya juu chini ili kumzingira, jambo ambalo katu halitafanikiwa." 

Sayyid Hassan Nasrullah

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, "Usiku huu (jana Jumatatu) na leo Jumanne tutawaonyesha Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu kwamba sisi sio watu wa kubabaishwa na mizingiro, vikwazo, mashinikizo, njaa au umasikini." 

Sayyid Hassan Nasrullah leo Siku ya Ashura anatazamiwa kutoa hotuba inayohusu matukio ya hivi karibu ya siasa katika eneo hili la Asia Magharibi.

Tags

Maoni