Sep 10, 2019 12:41 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah: Vita vyovyote dhidi ya Iran vina maana ya kufutwa Israel katika uso wa dunia

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema mbele ya mjumuiko mkubwa wa Waislamu waliofurika kwa ajili ya maombolezo ya Siku ya Ashura ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Husain AS kwamba, vita vyovyote vile dhidi ya Iran vitakuwa na maana ya kuangamizwa na kufutwa katika uso wa dunia, dola pandikizi la Israel.

Televisheni ya al Alam imenukuu Sayyid Hassan Nasrullah akisema hayo leo Jumanne katika hotuba yake ya Siku ya Ashura na kusisitiza kwa mara nyingine kwamba, kambi ya muqawama itaendelea kuwa pamoja na wananchi wa Palestina na Yemen. Amesema, kile kinachoshuhudiwa hivi sasa kusini mwa Yemen ni ushahidi wa wazi kwamba wavamizi wa nchi hiyo yaani Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wanauangalia kwa jicho la tamaa utajiri wa Yemen lakini matokeo ya vita walivyovianzisha dhidi ya nchi hiyo si kitu kingine ghairi ya kushindwa na kupata aibu ya kihistoria wavamizi hao.

Mmoja wa mamluki wa wavamizi wa Yemen baada ya kuangamizwa na wanamapambano wa Kiislamu

 

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na Syria ni vya kidhulma na kusisitiza kwamba, baada ya kushindwa Israel katika vita vyake huko Paletina na Lebanon na kuendelea kushindwa magenge ya kigaidi na ukufurishaji katika nchi za Lebanon, Syria na Iraq, hivi sasa serikali ya Marekani haikuona njia nyingine isipokuwa kukimbilia kwenye vikwazo vya kifedha. 

Amesema, Hizbullah ya Lebanon itaendelea kuheshimu azimio nambari 1701 la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, muqawama na asasi nyingine zote za Lebanon zina haki ya kujihami na iwapo Israel itaivamia tena Lebanon, basi muqawama wa nchi hiyo uko tayari kutoa majibu makali na kwa muda unaofaa, na hakutakuwa na mstari wowote mwekundu kwenye majibu hayo.

Tags