Sep 11, 2019 03:26 UTC
  • Waislamu milioni tatu wazuru Haram ya Imam Hussein Karbala, wakumbuka mauaji yake

Zaidi ya Waislamu milioni tatu jana tarehe 10 Muharram ambayo ni maarufu kama siku ya Ashura, walishiriki katika maombolezo ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume wetu muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq.

Ripota wa televisheni ya al Aalam mjini Karbala amesema kuwa, Waislamu zaidi ya milioni tatu waliowasili Karbala hadi kufikia jana walishiriki katika marasimu na shughuli ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) na kutangaza tena uaminifu na utiifu wao kwa njia na malengo yake na kulinda umoja na mshikamano wa Waislamu. 

Waislamu hao ambao waliwasili Iraq kutoka maeneo mbalimbali ya dunia tangu tarehe Mosi Muharram wakijitayarisha kwa ajili ya maombolezo ya siku ya Ashura wamesisitiza tena kivitendo udharura wa Waislamu kutukuza na kuenzi matukufu yao na kushikamana barabara na mafundisho ya dini yao yaliyotekelezwa kivitendo na Imam Hussein na wafuasi wake katika siku ya Ashura kwa kupambana na dhulma na uonevu na kusimama kidete dhidi ya watawala madhalimu wasioheshimu ubinadamu na haki zao. 

Kumbukumbu ya mauaji ya Imam Hussein (as)

Imam Husseri bin Ali bin Abi Twalib ni mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) ambaye mtukufu huyo alimtangaza kuwa ni bwana wa vijana wa peponi. Imam Hussein aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 katika ardhi ya Karbala nchini Iraq akiwa pamoja na familia ya Mtume na masahaba zake wakipambana na jeshi la mtawala katili na dhalimu wa wakati huo, Yazid bin Muawiya.

Wakati huo huo Wizara ya Afya ya Iraq imetangaza kuwa wafanyaziara 32 wameaga dunia na wengine 108 wamejeruhiwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliotokea jana katika mlango wa Babul Rajaa ndani ya Haram ya Imam Hussein (as). 

Maafisa wa usalama wa Iraq wanasema vifo hivyo vimetokana na msongamano mkubwa wa watu katika eneo hilo.  

Tags