Sep 11, 2019 07:09 UTC
  • Nguvu za Muqawama katika maneno na vitendo

Mikwaruzano baina ya kambi ya muqawama na utawala wa Kizayuni wa Israel imezidi kuwa mikubwa katika miezi ya hivi karibuni huku makundi ya muqawama yakizidi kuonesha nguvu zao kupitia maneno na vitendo dhidi ya utawala huo pandikizi.

Hivi sasa Benjamin Netanyahu anashikilia vyeo viwili katika utawala wa Kizayuni, cheo cha Waziri Mkuu na kile cha Waziri wa Vita wa utawala huo dhalimu. Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, hasa baada ya kushindwa kuunda baraza jipya la mawaziri mwezi Mei mwaka huu, Netanyahu aliona amalizie hamaki zake katika kuzusha mizozo, mikwaruzano na vita kati yake na makundi ya muqawama. Hata hivyo majibu makali ya kambi ya muqawama dhidi ya chokochoko hizo za Netanyahu yamevuruga njama zake zote za kujaribu kujikwamua kutoka katika kinamasi, na kambi hiyo ya muqawama imeonesha nguvu zake kubwa kwa uwazi kabisa, katika maneno na matendo. 

Wanajeshi Wazayuni wakilizana na wakijificha wa woga kuhofia makombora ya muqawama

 

Nguvu za kambi ya muqawama katika maneno zinaonekana wazi. Ushahidi wa hayo umo kwenye matamshi ya Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aliyotoa katika usiku wa kuamkia Siku ya Ashura na mchana wa siku hiyo adhimu. Katika hotuba yake mchana wa Siku ya Ashura, Sayyid Hassan Nasrullah aliuponda vibaya uwezo wa kijeshi wa Israel na kusema: "Jeshi la maajabu na lisilolishindika la Israel, leo hii limegeuka na kuwa jeshi la Hollywood." Aidha aligusia nukta nyingine muhimu akisema: "Katika historia yetu ya mapambano na Israel, hii ni mara ya kwanza kwa Israel kuweka ukanda wa usalama ndani ya ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu, na si nje ya ardhi hizo." Katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia jana, Sayyid Hassan Nasrullah alizungumzia nukta nyingine mbili muhimu. Nukta ya kwanza ni kwamba kambi ya muqawama  imeweza vizuri kukabiliana na mashinikizo ya Marekani na utawala wa Kizayuni na kuthibitisha kivitendo kwamba, si vikwazo, wala umaskini, wala ukata unaoweza kuleta dosari ndani ya kambi hiyo.

Nukta ya pili ni kwamba, Sayyid Hassan Nasrullah alisisitiza kwamba, waliomo ndani ya kambi ya muqawama si watu wanaoendekeza mizozo na mifarakano baina yao, bali ni watu walioshikamana barabara katika umoja wao wakiwa wamepiga kambi chini ya uongozi wa busara ya Kiongozi Muadhamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei. Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alisisitiza kwa kusema: "Marekani, Israel na vibaraka wao wanafanya njama za kuizingira kila upande na kuivunjavunja kambi yetu kuu (yaani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), lakini kamanda wa kambi hiyo ni Imam Khamenei na kitovu cha kambi hiyo ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo kamwe haiwezi kusalimu amri kwa kuzingirwa, kusababishiwa njaa na kulazimishwa kuingia vitani, na sisi tulioizunguka kambi hiyo tuko tayari kuilinda hadi tone la mwisho la damu yetu." 

Makombora ya muqawama wa Palestina yanayoutia kiwewe utawala pandikizi wa Israel

 

Msimamo huo wa Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon unadhihirisha mambo mawili makuu. Kwanza ni kwamba ameonesha kuwa anatambua vyema umuhimu wa vita vya kisaikolojia katika mapambano na adui kama ambavyo pia hayuko tayari kuruhusu vita hivyo vya kisaikolojia viviathiri vikosi na makundi ya muqawama, hivyo anatoa hotuba na tahadhari za wazi na kutekeleza kivitendo indhari zake ili kuwadhihirishia maadui kuwa anachokisema anakitekeleza kivitendo.

Jambo la pili ni kwamba, maneno na vitendo vya Sayyid Hassan Nasrullah vinathibitisha wazi kuwa askari na vikosi vya muqawama vinafanya mambo yao kwa njia bora kabisa kutokana na kujipamba kwao kwa imani ya kidini. Hilo limeonekana wazi pale majibu yaliyoahidiwa na Sayyid Hassan Nasrullah dhidi ya Israel yalipotekelezwa katika siku ya kwanza kabisa ya mwezi wa Muharram na katika hotuba yake ya Jumatatu usiku, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alisema kwa kugogoteza kwamba: "Sasa imewathibitikia akina Trump na Netanyahu kwamba, sisi ni watu ambao tunafuata njia ya Imam Husain AS, hivyo vikwazo na mzingiro wa aina yoyote ile hauwezi kutia doa katika nia na azma yetu thabiti."

Tags

Maoni