Sep 11, 2019 12:01 UTC
  • Uturuki yalalamikia matamshi ya kijuba ya Benjamin Netanyahu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu amesema kuwa matamshi ya Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni kuhusiana na eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ni ya kibaguzi.

Çavuşoğlu ameongeza kwamba, ahadi ya Benjamin Netanyahu ya kuviunganisha vitongoji vya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo mengine ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, ni kielelezo halisi cha ubaguzi wa rangi. Akizungumza jana kwenye kampeni za uchaguzi, Netanyahu alisema kuwa, iwapo atashinda katika uchaguzi wa bunge utakaofanyika siku ya Jumanne ijayo (Septemba 17), basi vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na sehemu zingine muhimu za eneo hilo, vitaunganishwa na utawala wa Kizayuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu

Mbali na Uturuki, mataifa ya Jordan na Qatar nayo yametoa radiamali kali kufuatia matamshi ya Netanyahu na kusisitiza kuwa, ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, haziwezi kuunganishwa na Israel. Eneo la Quds Mashariki na Ukingo wa Magharibi limekuwa chini ya utawala vamizi wa Kizayuni tangu mwaka 1967.  Eneo la Ukingo wa Magharibi linakadiriwa kuwa na vitongoji 250. Aidha katika vitongoji hivyo wanaishi zaidi ya Mayahudi laki nne, ambapo kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa makazi yote ya Kizayuni katika maeneo hayo, yamejengwa kinyume cha sheria.

Maoni