Sep 17, 2019 02:32 UTC
  • Hizbullah: Kombora letu jipya linaweza kusambaratisha manowari yoyote

Harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon (Hizbullah) imesema kombora lake jipya lenye uwezo wa kulenga shabaha kwa umakini mkubwa linaweza kuharibu aina yoyote ya manowari na meli za kijeshi.

Picha na maelezo yaliyochapishwa na Hizbullah kwenye ukurasa wake wa Twitter kuhusu kombora hilo yameeleza bayana kuwa, kombora hilo jipya lina uwezo wa kuwaangamiza watu wote watakaokuweko kwenye meli husika ya kijeshi, sambamba na kuiharibu kikamilifu manowari yenyewe.

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimeakisi kwa kina juu ya uwezo mkubwa wa kombora hilo la ardhini hadi majini lililozinduliwa na Hizbullah ya Lebanon karibu mwezi mmoja na nusu iliyopita.

Kifaru cha Hizbullah kikivurumisha kombora

Siku chache zilizopita, makombora ya ulinzi wa anga ya harakati ya Hizbullah yaliitungua na kuiteketeza ndege isiyo na rubani ya ujasusi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye anga ya kitongoji cha al-Adisah mkoani An-Nabtiyyah kusini mwa Lebanon.

Duru za usalama ndani ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zimekiri kuimarika uwezo wa kujihami wa harakati za Kiislamu za Hizbullah ya Lebanon na Hamas ya Palestina.

Tags

Maoni