Sep 17, 2019 10:32 UTC
  • Radiamali ya Uturuki dhidi ya matamshi ya Netanyahu kuhusiana na Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uturuki amesema kuwa, matamshi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel kuhusiana na kutaka kuliunganisha eneo la Ukingo wa Magharibi na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ni ya kijeuri na kifidhuli.

Molud Chavosh-oglu amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi wanachama waJumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ulifanyika Jumapili ya juzi katika mji wa Jeddah nchini Saudi Arabia na kusisitiza kwamba, kama uma wote wa Kiislamu ungeonyesha radiamali, basi mipango, siasa na kiburi pamoja na ujeuri wa Marekani na Israel usingefikia hapa.

Hatua ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uturuki ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina ina umuhimu mkubwa. Hii ni katika hali ambayo, walimwengu wanataraji kuwasikia viongozi wa nchi zote za Kiislamu wakiwaunga mkono kivitendo wananchi wa Palestina pamoja na malengo yao matukufu. Ukweli wa mambo ni kuwa, kila mara kunapofanyika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), viongozi kadhaa wa nchi za Kiislamu hutoa matamshi makali dhidi ya Israel. Kundi jingine la baadhi ya viongozi wa nchi za Kiislamu huamua kunyamaza kimya.

Mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) uliofanyika Septemba 15, 2019

Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana utawala wa kibaguzi wa Israel siku baada ya siku umekuwa ukitoa matamshi ya kijuba na kifidhuli zaidi. Katika uwanja huo, Jumanne iliyopita Benjamin Netanyahu alisema katika kampeni za uchaguzi wa Bunge la Israel kwamba, iwapo atashinda na kuunda baraza jipya la mawaziri ataviunganisha vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyojengwa  Ukingo wa Magharibi na sehemu nyingine muhimu ya ardhi ya Palestina na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Licha ya kuwa matamshi hayo kimsingi aliyatoa kwa shabaha ya kutafuta kura, lakini hapana shaka kuwa, kutolewa matamshi kama hayo, kunaonyesha malengo ya utawala huo wa kibaguzi. Hapana shaka kuwa, Uturuki ni miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) zilizo amilifu katika uga wa kukabiliana na harakati za utawala wa kibaguzi wa Israel. Pamoja na hali hiyo, lakini inaonekana kuwa, viongozi wa serikali ya Ankara hutoa matamshi na kuonyesha misimamo dhidi ya Israel kulingana na zama na kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa ya nchi yao. 

Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, sera za kigeni za serikali ya Recep Tayyip Erdogan zimekuwa na mwelekeo unaoeleweka katika sera na ajenda za serikali. Kiasi kwamba, katika kipindi cha karibu miongo miwili iliyopita, suala la  kukuza mivutano na nchi jirani na kusukuma mbele gurudumu la la malengo yake liliwekwa katika ajenda za serikali ya Ankara. Miongoni mwa mifano ya wazi katika sera za kigeni za Uturuki ambayo tunaweza kuiashiria ni mvutano wa sasa wa nchi hiyo na nchi za Syria na Iraq kwa upande mmoja, na mvutano wake na Ugiriki na Cyprus kwa upande wa pili.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

Pamoja na hayo uhusiano wa kiuchumi wa Uturuki na pande inazovutana nazo umeendelea kuweko. Kuhusiana na hilo, Shira Efron, mtaalamu wa taasisi ya RAND anaandika: Uturuki na Israel zimeonyesha kuwa, zina maslahi mengi ya pamoja katika uga wa uchumi, biashara, ugaidi na ushirikiano wa nishati.

Ukweli wa mambo ni kuwa, licha ya hitilafu zilizopo baina ya Uturuki na utawala haramu wa Israel inapasa kusema kuwa, Uturuki ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiislamu ambayo mwaka 1949 iliutambua rasmi utawala wa kibaguzi wa Israel. Uhusiano wa kisiasa wa Uturuki na Israel ambao kkatika muongo wa 90 ulipanuka kwa namna ambayo haikuwahi kushuhudiwa, mwaka 2010, ulitumbuki9a nyongo, baada ya vikosi vya usalama vya Israel kuishambulia meli ya Flotilla iliyokuwa imebeba misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Gaza. Pamoja na hayo, lakini mwaka 2017, Tel Aviv na Ankara ziliafikiana kurejesha uhusiano wao katika hali ya kawaida.

Tags