Sep 18, 2019 07:49 UTC
  • Abdul-Salam: Damu ya wananchi wa Yemen ni 'nzito' kuliko mafuta ya Saudi Arabia

Msemaji wa Harakati ya Wananchi wa Yemen ya Ansarullah ameitaka jamii ya kimataifa kulaani jinai za Saudia Arabia huko Yemen badala ya kuwalaumu Wayameni kwani damu za wananchi hao ni nzito na zenye thamani zaidi kuliko mafuta ya Saudia.

Muhammad Abdul-Salaam amesema hayo katika majibu yake kwa lawama dhidi ya Wayameni kutokana na mashambulio dhidi ya shirika la kusafisha mafuta la Saudi la Aramco na kusisitiza kwamba, kama Saudia haitasitisha hujuma na mashambulio yake ya kijeshi dhidi ya Yemen, basi operesheni zijazo za mashambulio dhidi ya muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh zitakuwa chungu na zenye maumivu zaidi.

Kiongozi huyo wa Ansarullah amewataka wale wanaotaka kuuweko uthabiiti na utulivu katika soko la mafuta waitake Saudia na washirika wake wasitishe uvamizi na mzingiro wao dhidi ya wananchi wa Yemen; kwani kinyume na hivyo kama damu ya wananchi wa Yemen itaendelea kuvunjiwa heshima basi matokeo ya jambo hilo yatakuwa mabaya.

Vituo vya kusafishia mafuta vya ARAMCO vikiteketea kwa moto baada ya kushambuliwa na wanamapambano wa Yemen

Jumamosi iliyopita, kikosi cha ndege zisizo na rubani kwa kushirikiana na kamati za wananchi, kilirusha ndege 10 zilizotengezwa na Wayemen, na kushambulia vituo vya kusafishia mafuta vya Buqayq na Khurais, vinavyomilikiwa na Shirika la Kitaifa la Mafuta la Saudia ARAMCO na kusababisha hasara kubwa kwa Riyadh.

Wapenda haki kote ulimwenguni wameendelea kushangazwa na hatua ya baadhi ya nchi kulaumu majibu ya mashambulio ya wananchi wa Yemen dhidi ya uvamizi wa Saudi Arabia na kunyamazia kimya jinai za utawala huo ambazo zimekuwa zikiendelea kwa miaka kadhaa sasa.

Tags

Maoni