Oct 12, 2019 04:53 UTC
  • Wapalestina walaani mashambulizi ya Uturuki nchini Syria

Harakati ya Kidemokrasia kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina sambamba na kutoa taarifa ya kulaani uvamizi wa kijeshi wa Uturuki dhidi ya ardhi ya Syria kwa kuutaja kuwa uliokiuka haki ya kujitawala na uhuru wa nchi hiyo ya Kiarabu, imesisitiza kuwa mashambulizi hayo ni uingiliaji wa wazi wa Ankara katika masuala ya ndani ya Syria.

Kundi hilo la Palestina limezitaka nchi za Kiarabu kuiunga mkono Syria dhidi ya uvamizi huo wa Uturuki huku likiubebesha dhima ya kisiasa na kisheria Umoja wa Mataifa ili uweze kukomesha uvamizi huo. Katika uwanja huo, Mohammad Yusuf Dahlan, mmoja wa makamanda wa muqawama wa Palestina pia amelaani mashambulizi ya Uturuki dhidi ya Syria. Dahlan amesema kuwa mashambulizi hayo ya Uturuki ni katika silsila ya uvamizi wa mara kwa mara wa serikali ya Ankara dhidi ya Syria na Iraq. Wakati huo huo wanamgambo wa Kikurdi wanaojiita Syrian Democratic Forces (SDF) wameushambulia kwa mizinga mji mdogo wa Akçakale wa Uturuki. Kwa mujibu wa habari hiyo wanamgambo hao wa Kikurdi wametekeleza hujuma hiyo katika kujibu mashambulizi ya jeshi la Uturuki katika maeneo ya kaskazini mwa Syria.

Wapiganaji wa Kikurdi ambao wanapambana na Uturuki

Katika shambulizi hilo watu wawili wameuawa na wengine 13 kujeruhiwa, huku jengo moja la serikali ya Uturuki likishambuliwa kwa maroketi mawili na mizinga minne. Hii ni katika hali ambayo duru za habari nchini Syria zinaripoti kujiri mapigano makali kati ya wanamgambo wa Syrian Democratic Forces (SDF) na askari wa Uturuki karibu na mji wa Sari Kani kwa kutumia silaha nyepesi na za wastani. Wakati huo huo kundi moja linalojiita ‘Jeshi la Kitaifa’ ambalo ni sehemu ya askari watembea kwa miguu wa Uturuki, limetangaza kudhibiti vijiji viwili kando ya mji wa Tell Abiad, kaskazini mwa Syria.

Tags

Maoni