Oct 20, 2019 02:33 UTC
  • Maandamano ya watu wa Lebanon, makataa ya Hariri na ahadi za Jenerali Aoun

Miji mbali mbali ya Lebanon, ukiwemo mji mkuu wa nchi hiyo, Beirut, kwa siku kadhaa sasa imeshuhudia maandamano ya wananchi wanaolalamikia sera za kiuchumi za serikali ya Waziri Mkuu Saad Hariri.

Watu wa Beirut na miji mingine ya Lebanon, Alhamisi usiku walijitokeza kwa wingi na kuandamna kupinga kuongezeka kodi na hatua zingine za utawala wa Saad Hariri.

Huko nyuma pia Lebanon iliwahi kushuhudia maandamano mara kadha ya wananchi ambao wanalalamikia sera za kiuchumi za serikali na maandamano ya sasa pia ni ya kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi.

Maandamano ya watu wa Lebanon kwa kawaida huwa ya amani na kile ambacho huwa wanataka ni kutatuliwa matatizo ya kiuchumi na kuzingatiwa watu wenye pato duni na wasio na ajira katika jamii.

Kushiriki Walebanon katika maandamano mitaani mjini Beirut na hasa karibu na ofisi ya waziri mkuu kumemfanya Saad Hariri azungumze kwa njia ya moja kwa moja na wananchi waliokuwa wakilalamika.

Katika hotuba yake Ijumaa usiku, ambayo aliitoa ili kuwatuliza wananchi, Hariri aliwapa maafisa wa ngazi za juu wa mrengo wake serikalini muhula wa masaa 72 ili kuwasilisha njia za kutatua mgogoro ambao umejitokeza.

Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri

Mrengo wa chama cha Hariri katika serikali unajumuisha watu ambao ni matajiri wakubwa wa Lebanon na ndio waliopendekeza ongezeko la kodi na ushuru ili serikali iweze kupata pato jipya. Serikali ya Lebanon imekumbwa na tatizo la nakisi ya bajeti kutokana na madeni mengi ya kigeni na ongezeko la gharama mbali mbali.

Katika kubuni sera sahihi za kiuchumi nchini Lebanon, mrengo wa Hariri umekataa kuyashirikisha makundi mengine kama vile Hizbullah na hali kadhalika Saad Hariri anategemea kupita kiasi madola ya kigeni ambapo utawala wa Saudia umekiuka ahadi zake za kuipa serikali yake misaada ya kifedha. Hizo ni baadhi ya sababu ambazo zimepelekea hali ya mambo kuharibika na hivyo wananchi wamejitokeza mitaani kulalamika.

Kiujumla, hali ya Lebanon haijawa nzuri katika utawala wa Saadi Hariri. Ustawi wa kiuchumi  wa nchi hiyo umedorara na kufika kiwango cha chini ya asilimia moja, huku kukiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 6, madeni ya kigeni nayo yamefika dola bilioni 86, kuna asilimia 25 ya ukosefu wa ajira miognoni mwa vijana na takribani watu milioni mbili wanaishi chini ya mstari wa umasikini katika nchi yenye idadi ya watu milioni 6. Matatizo hayo yameongezeka kufuatia uamuzi wa serikali wa kuongeza kodi na ushuru na jambo hilo limewakasirisha sana wananchi ambao wamejitokeza mitaani kuandamana.

Ingawa matakwa ya wananchi wa Lebanon ni halali na yanayoeleweka lakini baadhi ya watu wanataka kuyatumia vibaya na kuanza kuyatuhumu makundi mengine ili kufikia malengo yao ya kisiasa. Lengo la kutumia mbinu kama hiyo ni kuvuruga umoja na mshikamano katika jamii ya Lebanon yenye kaumu kadhaa.

Kuhusiana na hili, Gebran Bassil Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Ijumaa usiku alisema: "Baadhi wanataka kutumia vibaya hisia zenye nia njema za wananchi ili kufikia malengo yao ya kisiasa, yaani kuvuruga maelewano ya kitaifa ya serikali na bunge."

Rais Michel Aoun wa Lebanon

Muundo wa kijamii wa Lebabon ambao unajumuisha makabila kadhaa na makundi mbali mbali ya kisiasa unapelekea kuwepo na hatari ya kuibuka makabiliano ya wenywe kwa wenyewe katika nchi hiyo ambayo miaka ya nyuma iliwahi kushuhudia vita vya ndani.

Kwa kuzingatia hali hiyo, kwanza kuna haja  ya kujiepusha na michezo ya kisiasa na pili kuna udharura wa kuanzishwa  jitihada maradufu na za pamoja za serikali na bunge, mihimili miwili ambayo inawakilisha irada ya makundi mbali mbali ya nchi hiyo, ili uwezo wa ndani ya nchi utumiwe kuyatafutia suluhisho matatizo yaliyopo na hivyo kutekeleza matakwa ya wananchi na kuimarisha uchumi wa Lebanon.

Ni kwa kuzingatia nukta hizo ndipo Rais Michel Aoun wa Lebanon Ijumaa usiku akakutana na baadhi ya wawakilishi wa waandamanaji na kusema: 'Nitafanya yote ninayoweza ili kutatua matatizo ya watu wa Lebanon."

 

Tags

Maoni