Oct 21, 2019 07:10 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah, mwanasiasa mpenda mageuzi

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah Ijumaa iliyopita alitoa hotuba kwa mnasaba wa Arubaini ya Imam Hussein bin Ali Abi Twalib (as) akiunga mkono malalamiko ya wananchi wa Lebanon na kuendelezwa kazi za serikali ya sasa ya nchi hiyo sambamba na kutoa wito wa kufanyika marekebisho ya kisiasa.

Hotuba hiyo ya Sayyid Nasrullah ilikuwa na maudhui kadhaa muhimu. Kwanza kabisa ni kuunga mkono haki ya wananchi ya kufanya maandamano na kupinga ushuru na kodi mpya zilizowekwa na serikali. Kuhusiana na suala hilo Sayyid Nasrullah amesema: "Ujumbe wa malalamiko haya ni kwamba wananchi hawawezi kustahamili kodi mpya, na makundi ya kisiasa pia hayawezi kuzuia maandamano na malalamiko yao dhidi ya serikali."

Nukta ya pili ni uungaji mkono wa Katibu Mkuu wa Hizbullah kwa suala la kendelea kuwepo serikali ya sasa ya Lebanon. Sayyid Nasrullah amesema: "Hizbullah haitaki kuona serikali inajiuzulu." Kwa hakika ni kwamba Sayyid Nasrullah anatanguliza na kutoa kipaumbele kwa maslahi ya taifa na kupinga maandamano dhidi ya serikali yanayofanywa kwa ajili ya kuyanufaisha baadhi ya makundi ya kisiasa. Sayyid Nasrullah anaona kuwa, kujiuzulu serikali ya Lebanon katika kipindi cha sasa ni kupoteza wakati wa kushughulikia matatizo ya wananchi na wakati huo huo kunaweza kuiingiza nchi hiyo katika ombwe wa kisiasa na kutokuwa na baraza la mawaziri. Uungaji mkono huo wa Hizbullah kwa serikali ya Saad Hariri unashuhudiwa wakati Hariri mwenyewe hana msimamo mzuri kuhusiana na harakati hiyo ya mapambano na mara nyingine amekuwa akiikosoa Hizbullah katika mazungumzo yake na maafisa wa nchi za nje akizitaka nchi za kigeni kuiwekea mashinikizo zaidi. Kwa msingi huo msimamo wa sasa wa Katibu Mkuu wa Hizbullah unaonesha kuwa, hataki kulipiza kisasi kisiasa, na jambo muhimu zaidi kwake ni kuona amani na utulivu ukitawala nchi hiyo. 

Sayyid Hassan Nasrullah

Nukta ya tatu kuhusiana na hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah ni suala la "insafu ya kisiasa". Kwani licha ya kukiri kwamba, Lebanon inasumbuliwa na tatizo kubwa la kiuchumi na kwamba inaweza kukabiliwa na mporomoko au hata kusambaratika kiuchumi, lakini amesisitiza kuwa: "Hali ya sasa ya Lebanon si matokeo ya kazi na hatua za serikali ya sasa au matunda ya mwaka mmoja au kipindi maalumu, bali kwa uchache ni mjumuiko wa matatizo ya kipindi chote cha miaka 30 iliyopita; kwa msingi huo sisi sote tunabeba dhima, na si sahihi kwa baadhi ya watu waliokuwa katika serikali zote zilizopita kupanda mawimbi ya malalamiko ya wananchi na kutoa wito wa kupambana na ufisadi." Msimamo huu unaonesha umahiri na ustadi mkubwa wa kisiasa wa Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah.

Nukta ya nne katika hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah ni matamshi yake kuhusu kuwepo ufisadi nchini Lebanon. Sayyid Nasrullah anaamini kwamba, ufisadi na ubadhirifu wa mamilioni ya dola vinawafanya wananchi wapoteze imani yako kwa serikali. Anasema kwamba, katika kipindi cha sasa Lebanon inasumbuliwa na mgogoro wa wananchi kutokuwa na imani na serikali, na kwa njia isiyo ya moja kwa moja anaashiria kwamba, hicho ndicho chanzo kikuu cha malalamiko ya sasa dhidi ya serikali ya Beirut. Kwa msingi huo Katibu Mkuu wa Hizbullah ameishauri serikali kubadili sera zake na kufanya jitihada za kurejesha imani ya wananchi.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon

Nukta ya mwisho ni kuwa, mwenendo huo wa Sayyid Hassan Nasrullah ni kielelezo cha "mwanasiasa mmpenda mageuzi" ambaye anaweza kuwa kigezo bora cha kufuatwa na baadhi ya watawala na wanasiasa katika nchi mbalimbali duniani.       

Maoni