Oct 21, 2019 12:49 UTC
  • Ushirikiano wa Bahrain na utawala wa Kizayuni chini ya mwavuli wa muungano wa Marekani

jana Jumapili, Bahrain ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa siku mbili uliokuwa na ajenda ya kulinda usalama baharini.

Duru za habari zilisema kuwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel pia ulishiriki mkutano huo wa usalama wa baharini chini ya usimamizi wa Marekani. Kikao hicho abacho kilihudhuriwa pia na Saudi Arabia, Imarati, Kuwait na Oman, kidhahiri kilikuwa na lengo la kujadili masuala ya kiusalama. Usalama wa baharini si maudhui inayozihusu nchi chache tu za eneo, bali nchi zote zinazohusika kwa njia moja au nyingine na usalama wa bahari na safari za meli katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Hata hivyo kikao cha Bahrain ni sehemu ya muendelezo wa harakati za kuidhihirisha Iran kuwa nchi hatari na tishio kwa usalama wa eneo. Kikoa hicho ni sehemu ya kikao kikuu kilichofanyika hapo mwezi Februari mwaka huu huko Warsaw, mji mkuu wa Poland kwa usimamizi wa Marekani. Akthari ya shakhsia wa Marekani na nchi za Magharibi waliutaja mkutano wa Warsaw kuwa uliofeli, wa fedheha na wa kioja. Pamoja na hayo hivi sasa Bahrain kupitia chokochoko mpya, inakusudia kuendeleza harakati hizo za kichochezi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sambamba na mkutano huo, matamshi ya kijeuri ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain kuhusiana na harakati hizo zilizoratibiwa na Marekani, utawala haramu wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo, yanaakisi wazi ukweli huo. Katika kukaribia kufanyika kikao hicho, Khalid bin Ahmed Al Khalifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain alitoa matamshi yasiyo na ushahidi wowote kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaingilia mambo ya ndani ya nchi yake na kutuma nchini humo silaha na mada za miripuko.

Khalid bin Ahmed Al Khalifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain

Aidha Abdullah bin Rashid Al Khalifa, Balozi wa Bahrain nchini Marekani kupitia makala iliyochapishwa na gazeti la Washington Times alisema kuwa, sambamba na kikao hicho mjini Manama, kutafanyika pia maneva ya kimataifa ya siku mbili baharini kwa uongozi wa Marekani. Alisisitiza kuwa, lengo la kikao hicho ni 'kuunga mkono uhuru wa misafara ya meli na safari za kibiashara baharini na pia kufahamu vitisho vinavyotokana na Iran.' Inafaa kuashiria kuwa katika miezi ya hivi karibuni eneo la Ghuba ya Uajemi limekumbwa na migogoro na mizozo ambayo sababu na chanzo chake kiko wazi. Uharamia wa baharini na vitisho dhidi ya usalama wa meli na pia kuzuia usafirishaji huru wa nishati ya mafuta, ni miongoni mwa maudhui ambazo zinatokana na uingiliaji wa madola ya kigeni katika eneo la Asia Magharibi sambamba na kuanzisha kambi za kudumu na kuwepo kijeshi Marekani katika eneo hili. Ali Rahim Pur, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema katika uchambuzi wake wa siasa za Marekani Asia Magharibi: "Marekani katika kushadidisha mashinikizo dhidi ya Iran na kuendesha propaganda zenye lengo la kuidhihirisha nchi hii kuwa ni tishio, inafuatilia malengo mawili. Kupitia siasa hizo Marekani inapata kununua mafuta kwa bei nafuu kutoka nchi za Ghuba ya Uajemi na pia kuzuizia silaha zake.

Ushirikiano wa Bahrain na utawala haramu wa Israel

Kwa hakika mgogoro ulioibuka katika eneo unadhmini maslahi ya nchi za Magharib." Ni suala lililo wazi kwamba siasa za Marekani ambazo zinaenda sambamba na kuibua mizozo katika eneo, zinaandaa mazingira ya uwepo wake kwa ajili ya kutekeleza malengo na mipango yake. Katika uwanja huo, Abdel Bari Atwan mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa ameutaja mwenendo huo kuwa ni mtego mpya kwa nchi za ukanda wa Ghuba ya Uajemi iliotegwa kwa kisingizio cha kukabiliana na 'hatari ya Iran.' Naye kwa upande wake Meja Generali Abdulrahim Mousavi, Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akizungumza kwenye marasimu ya hivi karibuni ya 'Malik Ashtar' sambamba na kuashiria njama za Marekani za kuanzisha muungano katika Ghuba ya Uajemi alisema: "Hata kama kufikiwa muungano huo ambao unafuatiliwa na Marekani ni ndoto tu, lakini iwapo utathibiti, utakuwa ni mpango mwingine mpya wa kishetani ambao bila shaka utaibua machafuko na kuzidhuru moja kwa moja nchi za eneo hili na zile zinazotegemea mafuta ya eneo hili." Uwepo wa Marekani katika eneo na ushirikiano wa baadhi ya tawala za Kiarabu na nchi hiyo ya Magharibi inayoendelea kuzua mizozo, haujakuwa na matunda mengine ghairi ya kuvuruga usalama wa eneo la Asia Magharibi. Sisitizo la Marekani la kuundwa muungano wa baharini katika eneo, pia linatolewa ili kufikia malengo hayo hayo.

Maoni