Nov 06, 2019 07:55 UTC
  • Kuwait yazifikishia Saudia na Bahrain ujumbe wa amani kutoka Iran

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait Khaled al-Jarallah amesema nchi yake imezifikishia Saudi Arabia na Bahrain ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kutaka amani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Kwa mujibu wa Shirika Rasmi la Habari la Kuwait (KUNA),  Khaled al-Jarallah amesema: "Kuwait imewakabidhi wakuu wa Saudia na Bahrain ujumbe huo lakini hadi sasa hakuna jibu lililotolewa."

Hivi karibuni pia gazeti la Al Jarida la Kuwait liliandika kuwa, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameziandikia barua Saudi Arabia na Bahrain na kwamba Kuwait ndiyo iliyokuwa na jukumu la kufikisha barua hizo.

Ali Rabie, msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema habari hiyo ya Al Jarida ni kweli  na kwamba Rais Hassan Rouhani amemtumia barua mfalme wa Saudia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitaka kuwa na uhusiano wa kirafiki na majirani zake na inaamini kuwa amani katika eneo inaweza kupatikana tu kupitia ushirikiano wa nchi za eneo. 

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait Khaled al-Jarallah 

Mnamo Septemba 25, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasilisha mpango mpya wa amani katika eneo la Ghuba ya Uajemi ambao unajulikana kama 'Ubunifu wa Amani wa Hormuz' kwa kifupi HOPE katika hotuba yake kwenye mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York.

Nchi kadhaa tayari zimetangaza kuunga mkono mpango huo wa amani wenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kieneo kwa ajili ya kulinda amani na uthabiti katika Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Lango Bahari la Hormuz. Mpango huo unalenga kushirikisha nchi za kieneo na kuzuia madola ajinabi kuingilia mambo ya eneo hilo.

Tags