Nov 14, 2019 08:01 UTC
  • Utawala wa Kizayuni; utawala wa kigaidi na wa mauaji ya makusudi

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, usiku wa kuamkia siku ya Jumanne ya tarehe 12 Novemba ulifanya shambulio la kigaidi kwa lengo maalumu katika eneo la Ukanda wa Gaza lililomlenga na kumuua shahidi Baha Abu al-Ata, mmoja wa makamanda wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina. Wakati huohuo, Wapalestina wengine zaidi ya 20 waliuliwa shahidi na wengine wengi wakajeruhiwa katika mashambulio mengine yaliyofanywa siku ya Jumanne, na utawala huo haramu.

Nukta ya kwanza kuhusu mauaji ya kigaidi ya Baha Abu al-Ata ni kwamba, mauaji hayo yalikuwa mpango ulioratibiwa na kutekelezwa kwa makusudi. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema, tangu siku 10 zilizopita, baraza zima la mawaziri la utawala huo wa Kizayuni liliafiki kwa kauli moja kuuliwa kigaidi Abu al-Ata. Ndio kusema kuwa, kitendo hicho cha kigaidi ni kielelezo cha wazi cha ugaidi wa kiserikali uliofanywa na utawala wa Kizayuni.

Shahidi Baha Abu al-Ata

Nukta ya pili ni kwamba, baada ya kumuua kigaidi Abu al-Ata, viongozi wa utawala wa Kizayuni wamejaribu kuonyesha kuwa kitendo hicho kilikuwa cha kijeshi kilichotokea katika mapigano na makabiliano ya utumiaji silaha. Kwa sababu hiyo, baadhi ya vyombo vya habari vya Israel vimetangaza kuwa, uamuzi wa kumuua kigaidi Abu al-Ata ulichukuliwa kutokana na kuhusika kwake katika mashambulio ya makombora yaliyofanywa dhidi ya Israel. Madai hayo yanatolewa ilhali hakuna mapigano yoyote yaliyotokea katika wiki za karibuni kati ya Israel na makundi ya muqawama ya Palestina. Ukweli ni kwamba, madai hayo yametolewa ili kukabiliana na hatua yoyote inayoweza kuchukuliwa na Palestina ya kufikisha malalamiko katika taasisi za kimataifa.

Nukta ya tatu ni kuwa, mauaji ya kigaidi ya shahidi Abu al-Ata yamefanywa wakati utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ukiwa umekwama katika suala la kuunda serikali; na kwa upande mwingine zikiwa zimepita siku mbili tu tangu kutangazwa Naftali Bennett kuwa waziri wa vita wa utawala huo ghasibu. Kuhusiana na nukta hiyo, kiongozi wa orodha ya pamoja ya wabunge Waisrael na Waarabu amesema, Netanyahu anatumia kila mbinu ili kuweza kuendelea kubakia madarakani. Na hasa ikizingatiwa kuwa Netanyahu mwenyewe ametamka na kukiri kuwa amemteua Bennett ili kumzuia asijiunge na mrengo wa mshindani wake wa kisiasa Benny Gantz.

Maandamano ya kulaani ugaidi wa Israel

Nukta ya nne ni kwamba, utawala wa Kizayuni, na hasa kwa muda wa mwaka mmoja sasa, umefikia hitimisho kuwa, kufanya hujuma na mashambulio kiholela ya kijeshi dhidi ya makundi ya muqawama hakutauwezesha kupata unayoyakusudia. Kwa hiyo ili kufidia vipigo na kushindwa kwake kijeshi, umeamua kutumia mbinu ya kuwaua kigaidi viongozi na makamanda wa Kipalestina. Kuhusiana na suala hilo, gazeti la Haaretz liliandika katika toleo lake moja la mwezi Agosti kuwa, badala ya kufanya hujuma kubwa na za kila upande dhidi ya Gaza, Israel imekusudia kutumia tena sera ya kuwaua kigaidi viongozi, hasa wa muqawama wa Palestina. Ripoti iliyotolewa katika toleo hilo la Haaretz ilibainisha kuwa, mazingira ya utekelezaji wa sera hiyo yamepatikana, baada ya jeshi la utawala haramu wa Israel na shirika la usalama la utawala huo wa Kizayuni, Shin Bet kila moja kutangaza kwa upande wake kuwa, linafadhilisha kutumia sera ya kuwaua kigaidi viongozi wa muqawama badala ya operesheni kubwa za mashambulio ya kijeshi.

Nukta ya tano ni kwamba, kuuliwa kigaidi shahidi Abu al-Ata kutaugharimu na kuuhasiri mno utawala wa Kizayuni. Abu Mujahid, mmoja wa makamanda wa brigedi za Palestina amesema: Shambulio la kumuua kigaidi Abu al-Ata na njama ya kumuua kigaidi pia Akram al-Ajuri, afisa mwandamizi wa harakati ya Jihadul-Islami, maana yake ni kuanzisha vita na mapigano mengine mapya na muqawama. Mkuu wa ofisi ya habari ya Jihadul-Islami ya Palestina, yeye amesisitiza kuwa: Mauaji ya kigaidi ya Baha Abu al-Ata, kamanda wa tawi la kijeshi la Harakati ya Jihadul-Islami ni sawa na utawala ghasibu wa Israel kutangaza vita dhidi ya Wapalestina.

Makombora ya Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina

Kuhusiana na suala hilo, mara baada ya jinai hiyo iliyofanywa na Israel, makundi ya muqawama yalivurumisha makombora yapatayo 200 kuelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la Israel, na kusababisha Wazayuni zaidi ya 50 kujeruhiwa. Wakati huohuo hofu kubwa imetanda katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu, kiasi cha kuifanya Israel iamue kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014 kufunga shule na vituo vyake vyote vya umma. Aidha, vyombo vya habari vya utawala huo wa Kizayuni vimeripoti kuwa, wanafunzi milioni moja pamoja na walimu na wahadhiri elfu 80 wameamua kubaki majumbani na kukataa kwenda vyuoni na mashuleni kwa kuhofia mashambulio ya makombora ya makundi ya muqawama.

Nukta ya mwisho kabisa ni kuwa, jibu la makundi ya muqawama ya Palestina kwa mauaji ya kigaidi ya shahidi Abu al-Ata na kuvurumishwa makombora kadhaa kuelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni kielelezo cha haki ya kisheria ya kujihami waliyonayo Wapalestina, ambayo imebainishwa wazi katika kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo, mnamo siku zijazo tusishangae kushuhudia mapigano makubwa kati ya makundi ya muqawama na utawala wa Kizayuni, mapigano ambayo yanaweza kuathiri uundaji wa baraza jipya la mawaziri la utawala huo haramu.../

Maoni