Nov 15, 2019 01:23 UTC
  • Muhammad Al Houthi amkosoa Mjumbe Maalumu wa UN katika masuala ya Yemen

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amekosoa juhudi za Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen kwa ajili ya kuitisha mazungumzo kati ya harakati ya Ansarullah na muungano vamizi wa Saudi Arabia.

Muhammad Ali al Houthi ameashiria juhudi zinazofanywa na Martin Griffith kwa ajili ya kufanyika mazungumzo kati ya makundi ya Wayemeni na muungano vamizi unaoongozwa na Saudia na kueleza kuwa: Hakutapatikana njia ya kuhitimisha vita huko Yemen madhali muungano huo vamizi hauko tayari kwa mazungumzo.

Wakati huo huo, Faris al Himyari mwandishi habari wa Yemen ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, ujumbe wa kijeshi wa Saudi Arabia umekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Ansarullah mjini San'aa. 

Khalid bin Salman bin Abdulaziz mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ulinzi Jumatatu wiki hii aliwasili Muscat mji mkuu wa Oman katika safari ambayo haikutangazwa hapo kabla.  Baadhi ya duru zisizo rasmi zimeripoti kuwa safari ya Naibu Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia huko Muscat ni katika juhudi zinazofanywa na Riyadh ili kufikia mapatano na harakati ya Ansarullah ya Yemen. 

Mwana  Mfalme, Khalid bin Salman bin Abdulaziz, Naibu Waziri wa ulinzi wa Saudia 

Saudi Arabia ilikuwa ikipinga wito wa kusimamisha vita huko Yemen kabla ya taasisi za mafuta za nchi hiyo za kampuni ya Aramco kushambuliwa na jeshi la Yemen Septemba 14 mwaka huu. 

Tags

Maoni