Nov 16, 2019 02:42 UTC
  • Sababu za kujiuzulu serikali ya Kuwait

Waziri Mkuu wa Kuwait Jaber Al-Mubarak Al-Hamad Al-Sabah jana tarehe 14 Novemba alikabidhi hati ya kujiuzulu serikali yake kwa Amir wa nchi hiyo.

Mgogoro wa sasa wa Kuwait ulianza baada ya mbunge Saleh al Mulla kutoa wito wa kufanyika maandamano dhidi ya serikali katika mitandao ya kijamii. Maandamano hayo yamefanyika kwa ruhusa ya serikali kwa kaulimbiu ya "Inatosha".

Kunatajwa sababu kadhaa za kujiuzulu serikali ya Kuwait. Miongoni mwa sababu hizo ni maandamano makubwa ya wananchi. Maandamano hayo dhidi ya serikali yanafuatia yale yanayoshuhudiwa katika nchi za Iraq na Lebanon dhidi ya serikali za nchi hizo. Wakuwait wanalalamikia ufisadi mkubwa uliokita mizizi katika taasisi za serikali, utendaji udhaifu katika sekta ya ujenzi wa nyumba, afya na elimu na wanataka kufutwa kazi baadhi ya maafisa wa serikali na kufanyika marekebisho. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, sababu za maandamano ya Wakuwait zinashabihiana sana na zile za maandamano ya wananchi katika nchi za Iraq na Lebanon.

Jaber Al-Mubarak Al-Hamad Al-Sabah

"Mabedoon", wananchi wa Kuwait ambao uasili wao wa Kikuwait haujathibitishwa na kwa msingi huo bado hawatambuliwi kuwa ni raia wa nchi hiyo ndio waliokuwa wengi zaidi katika maandamano dhidi ya serikali. Cheche ya kwanza ya mandamano hayo ilikuwa kujiua vijana wawili kutoka tabaka la Mabedoon walioamua kuhitimisha uhai wao kutokana na hali mbaya ya maisha.

Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu wa Kuwait, Muhammad al Hamiidi anasema: "Maandamano ya Wakuwait yanafanyika kwa shabaha ya kutuma ujumbe kwa Bunge la Taifa na baraza la mawaziri na vilevile kupinga ufisadi. Maandamano haya hayakuchochewa na mrengo wowote wa kisiasa na wahusika ni wananchi wa kawaida wanaozongwa na matatizo ya nyumba, huduma za afya na matibabu na haki ya kupata elimu. Wananchi hawa wanaoandamana pia wanalalamikia na kupinga uuzaji wa makampuni ya serikali na uporaji wa mali ya umma unaofanywa na baadhi ya watu."

Maandamano ya wananchi wa Kuwait dhidi ya serikali

Kuwait ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani. Waandamanaji wanasema badala ya pato kubwa la mafuta la nchi hiyo kutumiwa katika kuboresha huduma za kijamii na hali ya kiuchumi ya wananchi, linatumiwa kwa maslahi ya watu binafsi wanaoshika madaraka ya nchi na jamaa zao wa karibu; kwa msingi huo ufisadi unaongezeka siku baada ya nyingine nchini humo. 

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, kwa kuzingatia kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu Jaber Al-Mubarak Al-Hamad Al-Sabah amekuwa madarakani tangu miaka 8 iliyopita, hivyo anawajibika mbele ya malalamiko ya sasa ya Wakuwait. Kwa msingi huo amekhitari kujiuzulu kama njia ya kuzima malalamiko hayo.

Sababu ya pili ya kujiuzulu serikali ya Kuwait ni hatua ya Bunge ya kuwasaili mawaziri wawili na kujiuzulu mwingine wa tatu. Jumatano iliyopita Bunge la Kuwait lilitangaza kwamba, litamsaili Waziri wa Huduma za Jamii Jenan Bushehri na Waziri wa Mambo ya Ndani Khaled Al Jarrah Al Sabah. Waziri wa Fedha wa Kuwait Dr. Nayef Al-Hajraf alijiuzuliu Ijumaa iliyopita ya tarehe 8 Novemba.

Kwa ufupi ni kwamba, Waziri Mkuu wa Kuwait amefikia natija kwamba Bunge la Taifa linakusudia kudhoofisha serikali yake na kwa msingi huo amechukua uamuzi wa kujiuzulu.

Alaa kulli hali maandamano kama haya ya sasa si jambo jipya nchini Kuwait na kubadilishwa baraza la mawaziri kunaweza kusimamisha na kusitisha malalamiko hayo.

Tags