Nov 16, 2019 02:45 UTC
  • Rais Bashar al-Assad: Syria katu haitagawanywa

Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema: Serikali ya Damascus haitaafiki kwa namna yoyote ile Syria igawanywe.

Rais wa Syria ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Russia-24. Bashar al-Assad amesema, genge la DAESH (ISIS) limejitokeza kwa matakwa ya Marekani na kuweza kuendesha harakati zake kwa uungaji mkono wa nchi hiyo; na akafafanua kwamba: Marekani ilikuwa inayatumia magaidi ya kundi la Daesh kama silaha ya kulilenga na kulihujumu jeshi la Syria.

Rais wa Syria ameongeza kuwa: Osama Bin Laden, Abu Bakr al-Baghdadi na mwasisi wa wanaoitwa askari wa kofia nyeupe imepasa wauawe kwa sababu muda wa matumizi yao umemalizika na wana siri muhimu ambazo haitakiwi zifichuliwe kwa sababu ni kwa madhara ya Marekani.

Osama bin Laden (kushoto) na Abu Bakr al-Baghdadi

Kuhusu Wakurdi wa Syria, Bashar al-Assad amesema: Kutokana na kuboreka uhusiano wa serikali ya Syria na Wakurdi wa nchi hiyo baada ya operesheni ya "Chemchemi ya Amani" iliyotekelezwa na Uturuki kaskazini mwa Syria, Marekani sasa inafanya kila njia kuzuia mazungumzo baina ya serikali ya Damascus na Wakurdi. Ameongeza kuwa: Marekani inataka kuwapiganisha Wakurdi na makundi mengine, lakini baada ya miaka saba ya vita, wananchi wengi wamebainikiwa na umuhimu wa kushirikiana na serikali halali ya Syria.

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo na televisheni ya Russia-24, Rais wa Syria amegusia pia makubaliano ya Sochi yaliyofikiwa na marais wa Russia na Uturuki na kusisitiza kwamba: Hivi sasa Uturuki inapaswa kuondoka katika ardhi ya Syria. Aidha, amesema kuwepo kijeshi Russia nchini Syria ni kwa ajili ya kupambana na ugaidi na kusisitiza kwamba, kuwepo huko kunaendana na mlingano wa kimataifa wa nguvu za kijeshi.

Bashar al-Assad pia ameeleza bayana kuwa, uwepo kijeshi wa Marekani nchini Syria ni wa uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu na akasisitiza kwamba: Kuwepo huko kwa Marekani kutaibua muqawama na hatimaye kutaifanya Washington ilazimike kuondoka na kupata hasara kubwa.../ 

Tags

Maoni