Nov 17, 2019 02:35 UTC
  • Kuwarejesha wanachama wa Daesh raia wa Ulaya; wenzo wa mashinikizo mapya wa Uturuki

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki imewafukuza Istanbul raia saba wa nchi za nje wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki imesema kuwa: Raia sita wa Ujerumani na mmoja wa Uingereza wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh wamerejeshwa katika nchi zao.  

Wanachama hao saba raia wa nchi za Ulaya wanachama wa kundi la Daesh wamefukuzwa na kurejeshwa makwao katika hali ambayo hivi karibuni serikali ya Ankara ilitishia kuwa, maelfu ya wafungwa wa Daesh watarejeshwa katika nchi zao iwapo nchi za Magharibi zitashindwa kutekeleza majukumu yao ya kifedha kwa serikali ya Uturuki, hata kama watakuwa wamevuliwa uraia wao. Serikali ya Ankara imekuwa ikizitishia mara kwa  mara nchi za Magharibi kwamba itafungua mipaka yake na kuwaruhusu wakimbizi na magaidi wa Daesh kurejea Ulaya. 

Kuhusiana na suala hilo, kabla ya hapo Suleyman Soylu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki alisema: "Uturuki si hoteli kwa ajili ya Madaesh na serikali ya Ankara itawarejesha makwao barani Ulaya wanachama wa kundi hilo la kigaidi raia wa kigeni. Vilevile serikali ya Ankara haikubaliani na matamshi ya viongozi wa nchi za Ulaya kuhusu kufutiwa uraia wanachama wa Ulaya wa kundi la kigaidi la Daesh na Uturuki inawarejesha wafungwa wa Daesh katika nchi zao."  

Kiongozi huyo wa serikali ya Ankara pia ameitaja hatua ya nchi za Ulaya kuhusu wakimbizi na wanachama wa Daesh raia wa nchi za bara hilo kuwa ni sawa na kukimbia majukumu na kusisitiza kuwa: Uturuki si hoteli kwa ajili ya mwanachama yoyote wa kundi la Daesh, na magaidi hao wanapasa kuondoka nchini.  

Suleyman Soylu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki 
 

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kamisheni ya Ulaya, raia wa nchi za Ulaya zaidi ya 5000 walijiunga na Daesh kati ya mwaka 2011 hadi 2016 yaani kipindi cha kupamba moto harakati na hujuma za kundi hilo kigaidi. 

Suala la kurejeshwa katika nchi zao magaidi wa Ulaya wanachama wa Daesh ni miongoni mwa daghadagha kuu za kiusalama zinazoukabili Umoja wa Ulaya. Ukweli wa mambo ni kuwa, nchi za Magharibi ambazo zimekuwa na mchango na nafasi muhimu katika kuliimarisha kundi la Daesh kwa shabaha ya kufanikisha maslahi yao huko Syria, Iraq na katika eneo la Asia Magharibi, hivi sasa zinakwepa kuwapokea magaidi hao wa Daesh ni raia wa Ulaya.  

Nukta ya kuzingatiwa hapa kuhusu jambo hilo ni vitisho vilivyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya nchi za Ulaya. Katikati ya mwezi Februari mwaka huu Trump alitangaza kuwa, Marekani na waitifaki wake wanawashikilia wanachama wa Daesh raia wa Ulaya zaidi ya 800 kutoka nchi za Ulaya hususan Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na  kuzitaka nchi hizo kuwapokea haraka iwezekanavyo magaidi hao. Trump aidha alizitishia nchi hizo za Ulaya kwamba Marekani itawaachia magaidi hao iwapo nchi hizo hazitawapokea.  

Rais Donald Trump wa Marekani 
 

Inaonekana kuwa, Uturuki na Marekani zinashirikiana kuhusu suala hilo la kuwarejesha wakimbizi wa Daesh barani Ulaya sambamba na kuziwekea mashinikizo nchi za Ulaya. Suala la kuwarejesha makwao wanachama hao wa Daesh mbali ya kuwa unyeti kiusalama na kisiasa, lina utata maalumu wa kisheria na serikali ya Ankara inalazimika kuondokana na shari hiyo haraka iwezekanavyo.  

Kuhusiana na suala hilo, inatupasa kusema kuwa, huwenda kuwarejesha katika nchi zao wanachama wa kundi la Daesh  kusiwe tatizo kubwa lakini jambo hilo halitakuwa jepesi kwa nchi kama Russia na Jamhuri zilizo chini ya udhibiti wa nchi hiyo na nchi za Asia ya Kati. Uturuki inakabilwa na matatizo makubwa zaidi katika kuwarejesha Madaesh wa Chechniya na Turkistan ya Mashariki au wale wa jamii ya Uyghur. Hii ni kwa sababu si jambo rahisi kwa Russia kuweza kudhibiti Chechnya au China kudhibiti maeneo ya Wayghur hasa kwa kutilia maanani kwamba nchi hizo mbili yaani Rusia na China  zina uhusiano mzuri na Uturuki. Suala hilo linaweza kutia dosari uhusiano wa kiuchumi na kiusalama wa Uturuki na Russia, China, nchi za Ulaya na Asia. 

Tags

Maoni