Nov 17, 2019 11:27 UTC
  • Katika hatua inayoonekana ni kusalimu amri, Bin Salman awasiliana kwa simu na Answarullah

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Yemen amesema kuwa, Saudia imeanza kufanya mawasiliano na Answarullah baada ya kushambuliwa viwanda vya mafuta vya Aramco vya Saudi Arabia.

Afisa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake ameliambia shirika la habari la Anadolu la Uturuki kwamba hivi sasa viongozi wa ngazi za juu wa Saudi Arabia wanafanya mawasiliano na viongozi wa Answarullah mkama vile mawasiliano ya simu yaliyofanywa na Khalid bin Salman, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Saudia na Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, Mahdi al Mashat. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pande mbili zimejadiliana njia za kusimamisha mapigano katika mipaka ya nchi hizo mbili.

Viwanda vya Shirika la Taifa la Mafuta la Saudia (ARAMCO) baada ya kuchakazwa vibaya na mashambulizi ya Answarullah

 

Afisa huyo wa Yemen ameongeza kuwa, mawasiliano baina ya pande hizo mbili yamekuwepo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na kwamba hivi sasa kumeundwa tume mbili, moja ya kijeshi na nyingine ya kisiasa. Ile ya kijeshi inatafua njia za kukomesha vita kikamilifu baina ya pande mbili, kuondolewa mzingiro wa Yemen na kufunguliwa uwanja wa ndege wa San'a wakati ile ya pili inaratibu hali mpya ya kisiasa nchini Yemen.

Katika upande mwingine, shirika hilo la habari la Uturuki limeripoti kuwa, hivi sasa Riyadh ndiyo inayohusika na kila linalotokea kusini mwa Yemen kiasi kwamba hata makubaliano ya Riyadh baina ya pande mbili hasimu za Yemen yatasimamiwa na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Khalid bin Salman ambaye hivi karibuni alikabidhiwa suala la Yemen kutoka mikononi mwa kaka yake, Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia.

Maoni