Dec 06, 2019 15:39 UTC
  • Maelfu ya Wapalestina wafurika kwenye haram ya Nabii Ibrahim kuzuia njama za Uyahudishaji

Maelfu ya Wapalestina walifurika katika haram ya Nabii Ibrahim eneo la Al-Khalil (Hebron) kutokana na mwito uliotolewa hapo kabla, ambapo walisali sala ya Alfajiri mahali hapo ili kuzuia njama za kuliyahudisha eneo hilo takatifu.

Awali wanaharakati wa wa Kipalestina ambao waliendesha kampeni waliyoipa jina la 'Alfajiri Kubwa' waliwataka raia wa Palestina kusali sala ya jamaa ya Alfajiri katika msikiti huo ili kutilia mkazo udharura wa haramu ya Nabi Ibrahim (as) kuendelea kubakia ya Kiislamu na pia kuilinda na uchu na tamaa ya utawala haramu wa Kizayuni ya kutaka kuliyahudisha eneo hilo. Baada ya maelfu ya Wapalestina kuingia msikitini humo walipiga takbira na nara nyingi za kidini kabla na baada ya kumaliza kusali. Mwezi Septemba mwaka huu, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala Haramu wa Kizayuni aliingia katika haram ya Nabi Ibrahim, kitendo ambacho kilipingwa vikali na Wapalestina.

Sehemu nyingine ya Waislamu wakisali msikitini hapo

Aidha mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, Reuven Rivlin, Rais wa utawala huo khabithi naye aliingia eneo hilo chini ya ulinzi mkali wa askari wa Israel. Baada ya mwaka 1994 ambapo mlowezi mmoja wa Kizayuni kwa jina la Baruch Goldstein, kuwashambulia Waislamu wa Palestina waliokuwa wakisali katika msikiti wa Nabi Ibrahim na kupelekea Waislamu 29 kuuawa shahidi, kamati ya Kizayuni inayoitwa 'Shemkaar' ilichukua hatua ya kutenga muda wa kuingia eneo hilo kwa Wapalestina na Wazayuni. Pamoja na hayo Wazayuni wamekuwa wakidhibiti viunga vyote vya msikiti huo katika sherehe zao sambamba na kuwazuia Waislamu kuingia eneo lao hilo. Kama hiyo haitoshi utawala haramu wa Kizayuni umechukua hatua ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo yanayoizunguka haram ya Nabii Ibrahim (as).

Tags

Maoni