Dec 07, 2019 07:42 UTC
  • Kushindwa kwa jitihada za Washington za kuanzisha uhusiano baina ya Morocco na Israel

Tangu aliposhika madaraka ya nchi miaka kadhaa iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani amechukua hatua ambazo hazijawahi kushuhudiwa za kuuhami na kuukingia kifua utawala wa Kizayuni wa Israel.

Miongoni mwa hatua hizo ni mikakati yake ya kutaka kuanzisha uhusiano baina ya utawala huo na nchi za Kiarabu. Katika uwanja huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ambaye baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu huko Ureno alielekea Morocco, hakuweza kuwasilisha pendekezo lake kwa viongozi wa nchi hiyo kuhusiana na suala la kuanzishwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili. Pompeo aliwasili Rabat Alkhamisi iliyopita na kukutana na Waziri Mkuu wa Morocco Saadeddine Othmani na vilevile Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Abdulatif Hamoushi. Ilipangwa kuwa baadaye Mike Pompeo angekutana na Mfalme Mohammed VI wa Morocco lakini mkutano huo umefutwa kwa sababu ambazo hazikutajwa. Vilevile Pompeo na mwenzake wa Morocco Nasser Bourita wamefuta mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari waliokuwa wamealikwa katika mkutano huo.

Mike Pompeo

Awali televisheni ya I24 ya utawala wa Kizayuni wa Israel ilikuwa imeripoti kuwa, safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani nchini Morocco inafanyika kwa shabaha ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya nchi hiyo na Israel. Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mapema jana alidai kuwa katika mazungumzo yake na maafisa wa Morocco Pompeo hakujadili suala la kuanzishwa uhusiano baina ya nchi hiyo na Israel.  

Hata hivyo ripoti za kuaminika zinaonesha kuwa, Mfalme Mohammed VI wa Morocco alikataa kukutana na Pompeo baada ya kutambua kwamba, alikuwa na nia ya kumshinikzia ili aanzishe uhusiano wa kidiplomasia na Israel.

Morocco ni miongoni mwa nchi za Kiarabu ambazo hazina uhusiano rasmi wa kidipmosia na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mwaka 2017 pia Mfalme wa Morocco alijiepusha kushiriki mkutano wa viongozi wa nchi za magharibi mwa Afrika ili asikutane na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Alaa kulli hal, licha ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kukanusha kuwa, safari ya Pompeo huko Morocco haikufanyika kwa shabaha ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hiyo na Israel lakini inaonekana kwa, serikali ya Donald Trump imekanusha ukweli huo baada ya Morocco kukataa matakwa yake. Katika safari hiyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amefanya jitihada za kutaka kuanzisha ufa katika ukuta mrefu unaozuia uhusiano wa kidiplomasia baina ya Israel na Morocco na kuiburuta zaidi Rabat upande wa utawala ghasibu wa Israel.

Donald Trump

Gazeti la Times la Israel limeandika kuwa, Netanyahu anataka kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Morocco kwa ajili ya kuimarisha nafasi yake ndani ya utawala huo. Vilevile kumetolewa ripoti nyingi kuhusiana na mikakati inayofanywa na Israel kwa shabaha ya kuanzisha uhusiano wa kisiasa na Morocco.

Serikali ya Donald Trump imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuanzisha uhusiano baina ya nchi za Kiarabu na Israel. Katika uwanja huo mtandao wa habari wa Axios wa Marekani wiki hii ulizinukuu duru za Israel na za Kiarabu zikisema kuwa: Naibu Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani wiki iliyopita alifanya mazungumzo na mabalozi wa Imarati, Morocco, Bahrain na Oman mjini Washington na kuwataka wasaini mkataba wa kutoshambuliana na Israel.

Licha ya jitihada kubwa za Trump za kuzitaka nchi za Kiarabu ziutambue rasmi utawala ghasibu wa Israel lakini inaonekana Marekani inakabiliwa na hali ngumu sana katika njia hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, jamii ya kimataifa na hata washirika wa Ulaya wa Marekani wanapinga sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ya Trump kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel.    

Tags