Dec 08, 2019 07:16 UTC
  • Ansarullah: Madai ya Marekani ya kukamata meli iliyobeba vipuri vya makombora hayana msingi wowote

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amesema, madai iliyotoa Marekani kuwa imekamata meli iliyobeba vipuri vya makombora yaliyokuwa yakipelekwa nchini humo hayana msingi wowote.

Jeshi la Wanamaji la Marekani limedai hivi karibuni kuwa limeikamata meli moja katika Bahari ya Kiarabu iliyokuwa ikielekea nchini Yemen, ikiwa imebeba vipuri vya makombora.

Muhammad Ali al-Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen, amekanusha madai hayo ya Marekani na kueleza kwamba, muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umefunga mipaka yote ya nchi kavu, baharini na ya anga ya Yemen na wala hauruhusu meli za mafuta au dawa ziingie nchini humo; sasa inakuwaje meli iliyobeba vipuri vya makombora inaweza kuingia huko Yemen.

Ndege za kivita za Saudia zinazofanya hujuma na jinai nchini Yemen

Al-Houthi ameashiria misaada ya silaha ya Marekani kwa muungano wa Saudia katika hujuma na mashambulio yake dhidi ya Yemen na kueleza kwamba: Gaidi halisi ni Marekani inayowawekea mzingiro na kuwaua wananchi wa Yemen.

Aidha mkuu huyo wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amezitaka Saudia na Imarati zikomeshe mashambulio yao na mzingiro zilioiwekea nchi hiyo.

Kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa, Saudi Arabia iliivamia kijeshi Yemen mwezi Machi mwaka 2015 na kuiwekea mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani nchi hiyo masikini ya Kiarabu ambao ungali unaendelea hadi sasa.../ 

Maoni