Dec 08, 2019 07:26 UTC
  • Nukta tano kuhusu jaribio la kombora la utawala wa Kizayuni wa Israel

Msemaji wa Jeshi la Utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 6 Disemba alitangaza kuwa jeshi la utawala huo lilifanyia jaribio kombora moja katika eneo la Ashdod.

Idara ya Habari katika Wizara ya Vita ya Utawala wa  Israel imetangaza kuwa, jaribio hilo limefanyika katika kituo cha kijeshi katika eneo la ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati), ni utawala wa Kizayuni wa Israel pekee ndio ulio na silaha za nyuklia. Inakadiriwa kuwa Israel ina vichwa vya nyuklia baina ya 80 hadi 400. Jaribio la kombora ambalo lilifanywa na utawala huo Ijumaa lina uwezo wa kusheheni bomu la nyuklia.

Jaribio hilo la kombora la nyuklia la utawala wa Kizayuni la siku ya Ijumaa lina nukta tano muhimu.

Awali kabisa ni kuwa, utawala huo wa Kizayuni unalisukuma eneo la Asia Magharibi katika muelekeo wa malumbano ya kijeshi katika hali ambayo baadhi ya madola makubwa katika eneo la Asia Magharibi, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanataka eneo la Asia Magharibi lisiwe na silaha za nyuklia. Kwa jaribio hilo, utawala wa Kizayuni umeweza kuimarisha uwezo wa makombora yake kusheheni silaha za nyuklia.

Nukta ya pili ni kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel haufungamani hata kidogo na mikataba au kanuni za kimataifa. Utawala huo ghasibu si tu kuwa hauruhusu ukaguzi wowote wa kimataifa ufanyike katika vituo vyake vya nyuklia ambvyo vinaendesha shughuli kinyume cha sheria, bali pia umekataa kutia saini Mkataba wa Kuzuia Uundwaji na Usambazwaji Silaha za Nyuklia (NPT). Jaribio la kombora la nyuklia ambalo lilitekelezwa na utawala wa Kizayuni siku ya Ijumaa ni ishara ya wazi kuwa ukiukwaji na upuuzaji sheria za kimataifa ni kipaumbele kwa utawala huo.

Nukta ya tatu ni kuwa, majaribio ya makombora ya utawala wa Kizayuni yanafanyika katika fremu ya sera za utawala huo za kukarabati makombora yake. Kuhusiana na hilo, mwezi Julai, Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kushirikiana na Marekani lilifanyia jaribio ngao ya makombora ya balistiki inayojulikana kama Arrow 3 katika jimbo la Alaska nchini Marekani.

Kituo cha nyuklia cha Dimona cha utawala haramu wa Israel

Siku ya Ijumaa pia utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanyia majaribio ngao ya makombora inayojulikana kama 'Kombeo la Daudi' ambayo ilianza kutumiwa na utawala huo miaka miwili iliyopita lakini wakuu wa utawala wa Kizayuni bado wana wasiwasi kuhusu uwezo wa ngao hiyo.

Nukta ya nne ni kuwa, Jeshi la Utawala wa Kizayuni lilifanya jaribio la kombora hilo la nyuklia siku ya Ijumaa wakati ambao utawala huo hivi sasa uko katika mkwamo wa kisiasi kutokana na kushindwa kuunda baraza la mawaziri. Waziri mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu hivi sasa anakaribia mwisho wa maisha yake ya kisiasa na jaribio hilo la makombora ni katika jitihada za kutuma ujumbe kuwa, mkwamo uliopo wa kisiasa haujavuruga masuala ya usalama na kijeshi katika utawala huo. Aidha jaribio hilo la kombora la nyuklia ni mbinu ya Netanyahu kujaribu kuendelea kubakia madarakani.

Nukta ya tano ni kuwa, madola ya Magharibi hayajatoa tamko lolote kuhusu jaribio la kombora hilo la nyuklia la utawala wa Kizayuni na kwa msingi huo yanaonekana kuunga mkono hatua hiyo.

Waziri mkuu wa utawala bandia wa Israel Benjamin Netanyahu

Ni kwa msingi huo ndio, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika taarifa aliyotoa kufuatia jaribio la kombora la nyuklia la utawala wa Kizayuni wa Israel amezikosoa nchi za Magharibi kwa kupuuza jaribio hilo. Zarif ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa pamoja na Marekani kamwe hazilalamiki kuhusiana na maghala pekee la silaha za nyuklia katika eneo la Magharibi mwa Asia ambayo yana makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia lakini daima zinaghadhabika kuhusiana na silaha za kawaida za kujilinda za Iran."

Upuuzaji huo kwa mara nyingine unathibitisha kuwa, madola ya Magharibi yana undumakuwili na yana mtazamo ulio kinyume cha sheria kuhusu majaribio ya makombora au mipango ya nyuklia.

Tags

Maoni