Dec 09, 2019 02:41 UTC
  • Azimio la Kongresi ya Marekani dhidi ya uvamizi wa utawala wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi

Serikali ya rais Donald Trump imekuwa ikitekeleza hatua zisizo za kawaida katika uwanja wa kuunga mkono vitendo vilivyo kinyume cha sheria vya utawala haramu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina.

Miongoni mwa hatua hizo za serikali ya Marekani ni uungaji mkono wake rasmi kwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuyaunganisha maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (yaani Israel.) Hata hivyo mwenendo huo umekabiliwa na upinzani mkali wa walimwengu na hivi sasa umeshuhudiwa pia ndani ya bunge la Kongresi nchini Marekani. Katika uwanja huo Ijumaa iliyopita ya Disemba 6 mwaka huu, Baraza la Wawakilishi nchini humo sambamba na kupasisha azimio la kupinga kuunganishwa sehemu ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), kwa mara ya kwanza wabunge wa chama cha Democrat walitangaza wazi kupinga siasa za Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel pamoja na muungano wake wa mrengo wa kulia. Azimio hilo lilipitishwa kwa kura za ndiyo 226, mkabala wa kura 188 za hapana za wabunge wa Marekani. Hata kama azimio hilo halina uwezo wa kuishurutisha Israel, lakini limeonyesha upinzani mkubwa wa wabunge wa chama cha Democrat dhidi ya siasa za Benjamin Netanyahuu na muungano wake wa mrengo wa kulia. Aidha azimio hilo ambalo liliwasilishwa mwezi Aprili mwaka huu kwa hoja iliyowasilishwa na Alan Leventhal, mbunge wa jimbo la California kwa tiketi ya chama cha Democrat, limepingwa na wabunge wanne wa chama hicho, kama ambavyo pia limeungwa mkono na wabunge watano wa chama cha Republican. Wabunge wanne wa Democrat waliopinga azimio hilo ni Ilhan Omar, Rashida Tlaib, Alexandria Ocasio-Cortez na Ayanna Pressley.

Utawala khabithi wa Israel ukibomoa kwa dhulma nyumba za Wapalestina na kujenga mahala hapo vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Wabunge hawa wana historia ya kuwa na misimamo ya kukosoa siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel. Rashida Tlaib amepinga azimio hilo kutokana upinzani wake kwa mpango wa uundwaji wa nchi mbili za Palestina na Israel. Na wabunge watatu wengine pia wamelipigia kura ya 'hapana' azimio hilo kutokana na kuwa na vipengee vyepesi kama vile kutotumiwa neno 'uvamizi' kwenye hati ya mwisho ya azimio hilo. Azimio hilo lililopitishwa katika Kongresi ya Marekani haliwezi kwa mtazamo wa kisheria kuzuia uungaji mkono wa serikali ya Washington kwa kadhia ya kuyaunganisha baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Pamoja na hayo azimio hilo linaonyesha kutokuwa radhi wawakilishi wengi wa chama cha Democrat na waungaji wao mkono kwa utawala haramu wa Kizayuni pamoja na siasa na hatua zake ovu dhidi ya Palestina. Wakati huo huo, uungaji mkono wa Wademocrat kwa azimio hilo, unaonyesha kuwa hatua yoyote katika uga wa kupenda kujitanua utawala khabithi wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi, ikiwemo hatua ya kuviunganisha vitongoji na maeneo yake na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), inaweza kuusababishia matatizo makubwa utawala huo wa Kizayuni kutoka kwa waungaji mkono wake wa Kimarekani. Kwa mujibu wa azimio hilo: "Pendekezo lolote la Marekani kwa ajili ya utatuzi wa mzozo uliopo kati ya Israel na Wapalestina, ni lazima lijumuishe upasishaji wa njia ya utatuzi wa kupatikana nchi mbili." Kwa upande mwingine, azimio hilo limepinga juhudi za Wapalestina kwa ajili ya kujipatia nchi yao huru bila kupitia mazungumzo na utawala haramu wa Kizayuni. Upasishaji wa azimio tajwa pamoja na kuwa na vipengee vyepesi, ni hatua ya wazi iliyo kinyume na uungaji mkono wa kila upande na usio na masharti wa serikali ya Rais Donald Trump kwa utawala wa Kizayuni. Katika uwanja huo, Novemba 18 mwaka huu, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alitangaza kwa mara nyingine uungaji mkono wa Washington kwa utawala wa Israel na kusema kuwa, kuanzia wakati huo, Marekani haitambui tena ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Ukongo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa unakiuka sheria za kimataifa.

Kwa mara ya kwanza Netanyahu na muitifaki wake Trump, wamepata pigo kubwa baada ya Kongresi kupinga ujenzi wa vitongoji vya walowezi

Akibainisha kuwa Marekani imebadili siasa zake kuhusiana na suala zima la ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, alidai kuwa, ujenzi huo wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kama ulivyo haukiuki sheria za kimataifa. Matamshi ya Pompeo yalikuwa yanakusudia kuvunja hati ya kisheria ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ya mwaka 1978. Kwa mujibu wa hati hiyo, ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo khabithi, unakinzana na sheria za kimataifa. Hii ilikuwa hatua mpya kwa serikali ya Marekani kutangaza uungaji mkono wake wa kila upande kwa hatua iliyo kinyume cha sheria ya utawala wa Kizayuni kama ambavyo inabainisha kwa mara nyingine njama endelevu za Washington kwa ajili ya kudhoofisha juhudi za Wapalestina za kutaka kutambuliwa taifa lao kwa anuani ya nchi huru. Ni vyema kuashiria pia kuwa tarehe 23 Disemba 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio namba 2334 ambalo liliutaka utawala khabithi wa Kizayuni ukomeshe mara moja shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Hata hivyo utawala huo umeendelea kukiuka azimio hilo sambamba na kuendeleza ujenzi wa vitongoji kwa lengo la kubadili muundo wa maeneo ya Palestina na kuyafanya kuwa miliki yake.

Tags

Maoni