Dec 09, 2019 12:23 UTC
  • Askofu Mkuu wa Kanisa la Othodoksi la Quds amuunga mkono Sayyid Hassan Nasrullah

Askofu Mkuu wa Kanisa la Othodoksi katika mji mtukufu wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) Atallah Hanna, ameiunga harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon sambamba na kulaani matamshi yaliyotolewa na Askofu wa Kanisa la Othodoksi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut, ya kuitusi harakati hiyo na Katibu Mkuu wake Sayyid Hassan Nasrullah.

Atallah Hanna amesema: Sayyid Hassan Nasrullah na Hizbullah ya Lebanon wametoa mchango muhimu katika kuwalinda na kuwahami Wakristo wa Syria na nchi zingine za Kiarabu; na Wakristo wote wa kanisa la Othodoksi katika nchi za Lebanon, Syria, Palestina na nchi nyingine za Kiarabu hawakubaliani na misimamo ya Askofu wa Kanisa la Othodoksi la Beirut.

Mufti wa Lebanon, Sheikh Ahmad Qablan, naye pia ametangaza kuwa: Hizbullah na Katibu Mkuu wake wameikomboa Lebanon, wameonyesha muqawama na wameirejeshea nchi iliyokuwa imevamiwa na kukaliwa kwa mabavu, uhuru, kujitawala na mamlaka yake.

Katibu mKuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah

Wakati huo huo, Muhammad Raad, kiongozi wa mrengo wa Al-Wafaa Lil-Muqawama katika bunge la Lebanon amesema, matamshi hayo ya kuitusi Hizbullah na Katibu Mkuu wake yanatolewa na mtu anayetaka kuzifumbia macho sababu halisi za mgogoro uliopo na kujaribu kuuandama muqawama wa Lebanon.

Ilyas Audah, Askofu wa Kanisa la Othodoksi la Beirut alitoa kauli ya kichochezi dhidi ya Sayyid Hassan Nasrullah na harakati ya Hizbullah katika misa iliyofanyika kwenye kanisa hilo jana Jumapili alipodai: Nchi hii (Lebanon) inaendeshwa na mtu ambaye nyote mnamjua; na kuna kundi pia linaitawala nchi hii kwa nguvu za mtutu wa bunduki.../

Tags

Maoni