Dec 10, 2019 14:22 UTC
  • Kuakhirishwa kikao cha Bunge la Lebanon; Saad Hariri katika ndoto za kurejea madarakani

Jumatatu ya jana tarehe 9 Disemba, ilipangwa kuwa Bunge la Lebanon likutane na kufanya mashauriano kuhusiana na Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo. Hata hivyo kikao hicho cha Bunge kiliakhirishwa.

Lebanon ilikumbwa na ghasia za maandamano ya wananchi kuanzia tarehe 17 Oktoba mwaka huu. Moja ya sababu kuu za kuibuka maandamano hayo, ni mgogoro wa kiuchumi pamoja na ufisadi mkubwa uliotawala katika ngazi tofauti za nchi hiyo ya Kiarabu, hususan katika uga wa masuala ya kifedha.

Kuendelea maandamano na malalamiko ya wananchi kulipelekea tarehe 29 Oktoba, Saad Hariri, Waziri Mkuu wa nchi hiyo ajiuzulu wadhifa wake huo. Hivi sasa zimepita zaidi ya siku 40 tangu Saad Haririi ajiuzulu, huku Waziri Mkuuu mpya akiwa bado hajapatikana. Waziri Mkuu wa Lebanon anapaswa kutoka katika jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni. Katika kipindi hiki cha zaidi ya siku 40, kumependekezwa majina mawili kwa ajili ya kushika wadhifa wa Waziri Mkuu.

Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon aliyejiuzulu

Awali Muhammad Safadi alipendekezwa kwa ajili ya wadhifa huo, hata hivyo akaamua kukaa kando kufuatia malalamiko ya waandamanaji. Katika kipindi cha juma moja lililopita kulikuwa kukiripotiwa habari ya kufikiwa maafikiano baina ya makundi ya Kilebanon kuhusiana na Samir al-Khatib kama mgombea mteule wa nafasi ya Waziri Mkuu na ilipangwa kuwa Bunge lingekutana jana Jumatatu na kufanya mashauriano ya mwisho kuhusiana na mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, Jumapili ya Juzi Samir al-Khatib akatangaza kujitoa na hivyo kupelekea kikao cha Bunge kwa ajili ya kuumjadili kuakhirishwa pia hapo jana Jumatatu.

Samir al-Khatib amesema kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba, sababu ya yeye kujiondoa ni kuweko ishara za Saad Hariri Waziri Mkuu aliyejiuzulu kutaka kurejea tena katika nafasi hiyo. Al-Khatib amesema bayana kwamba, alikutana na Sheikh Abdul-Latif Derian, Mufti Mkuu wa Waislamu wa Kisunni nchini Lebanon na kupitia mazungumzo yake akafahamu kwamba, natija ya mazunguumzo na mashauriano ni kuwa, Saad Hariri aarifishwe kwa ajili ya kuunda serikali ijayo ya Lebanon.

Sheikh Abdul-Latif Derian, Mufti Mkuu wa Waislamu wa Kisuni nchini Lebanon

Inaonekana kuwa, sababu kuu ya kutotangazwa Waziri Mkuu mpya wa Lebanon ni hamu na shauku ya Saad Hariri ya kurejea tena madarakani akiwa Waziri Mkuu. Hariri anaonyesha hamu hiyo katika hali ambayo, wakati anajiuzulu, Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon na Rais Michel Aoun wa nchi hiyo walikuwa miongoni mwa shakhsia waliokuwa wakipinga kujiuzulu Hariri na badala yake walimtaka awajibike mbele ya wananchi.

Muhammad Raad, Mkuu wa Mrengo Tiifu Kwa Muqawama Katika Bunge la Lebanon anasema kuwa, hatua ya kwanza ya kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi, ni kuundwa serikali amilifu na yenye kutambua majukumu ambayo itakuja na mbinu na mkakati mpya wa kupambana na ufisadi, kuwafungulia mashtaka mafisadi, kuyafanyia kazi mafaili ya ufisadi na kurejesha kwa wenyewe fedha zilizoporwa.

Saad Hariri anakusudia kutekeleza hivi sasa takwa na mpango wake aliouzungumzia kabla ya kujiuzulu nao ni kuunda serikali ambayo itakuwa na mamlaka zaidi ambapo wenye fikra na mitazamo mimoja na yeye wawe wengi katika serikali hiyo. Hii ni katika hali ambayo, wenye fikra na mitazamo ya pamoja na Saad Hariri katika Harakati ya Machi 14 walishindwa katika uchaguzi wa Bunge nchini Lebanon mwaka jana 2018.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah

Kuakhirishwa mara kwa mara uundwaji wa serikali ya Lebanon kuna taathira na matokeo matatu muhimu. Mosi, suala hilo linaandaa uwanja wa kurejea malalamiko na maandamanno, ambapo hilo limeshatokea ambapo kwa mara nyingine tena Lebanon imeshuhudiia maandamanao na kufungwa njia na barabara mbalimbali. Pili ni kuwa, vipaumbele na matakwa ya wananchi hayatapewa umuhimu

wa kwanza na Waziri Mkuu, kwani katika mwenendo huu inaonekana kuwa, kwa mara nyingine tena maslahi ya vyama na makundi yatabadilishwa na kuwa vipaumbele vya Waziri Mkuu. Tatu ni kuwa, matatizo ya kiuchumi ya serikali na wananchi wa Lebanon yatazidi kushadidi siku baada ya siku.

Katika uwanja huu na sambamba na kuendelea ombwe la serikali nchini Lebanon, hivi karibuni Saad Hariri aliwatumia barua viongozi wa nchi za Ujerumani, Italia, Uhispania, Ufaransa, Russia, Saudi Arabia, Uturuki, China na Uingereza, akiwaomba waisaidie Lebanon kifedha na pesa taslimu. Hii ni katika hali ambayo, gazeti la al-Jamhuriyyah linalochapishwa mjini Beiruti, hivi karibuni liliandika kuwa, madeni ya Lebanon yamefikia kiwango cha dola bilioni 90.

Tags

Maoni