Dec 14, 2019 07:25 UTC
  • Nasrullah: Hizbullah ni tishio kubwa kwa njama za Marekani na Israel

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema njama ghalati za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo zimekuwa zikigonga mwamba kutokana na uwepo na kusimama kidete harakati hiyo ya muqawama.

Sayyid Hassan Nasrullah alisema katika hotuba yake aliyoitoa jana Ijumaa kwa wafuasi wake kwa njia ya televisheni na kuongeza kuwa, "Hizbullah ni tishio kubwa kwa njama za Marekani na Israel katika eneo la Asia Magharibi."

Amesema Marekani inafanya juu chini kutaka kuonesha kuwa Hizbullah ni tishio kwa Lebanon, na kwamba njama zote hizo zinafanyika kwa ajili ya kupigania maslahi yake na ya utawala wa Kizayuni.

Sayyid Nasrullah ameeleza bayana kuwa, "Marekani haishughulishwi wala kuguswa na maslahi ya taifa la Lebanon. Washington inatoa mamilioni ya dola kwa ajili ya kuchafua taswira ya Hizbullah, lakini bila shaka njama hizo zitagonga mwamba."

Wanamuqawama wa Hizbullah ya Lebanon

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, Marekani na utawala haramu wa Israel zimekuwa zikipindisha matamshi yanayotolewa na viongozi wa Iran, ili kulichochea taifa la Lebanon dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa, harakati hiyo ya Muqawama imejiandaa kwa ajili ya kuusambaratisha kikamilifu utawala wa Kizayuni wa Israel, iwapo Tel Aviv itathubutu kuanzisha uvamizi au shambulizi lolote dhidi ya Iran. Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina uwezo wa kujihami na kujilinda, sambamba na kujibu mashambulizi tarajiwa ya Marekani na Israel.

Tags

Maoni