Dec 14, 2019 07:37 UTC
  • Ripoti: Saudia inafanya jitihada za kuboresha uhusiano na Iran

Gazeti la The Wall Street Journal la Marekani limeripoti kuwa, watawala wa Saudi Arabia wanafanya jitihada za chini kwa chini za kuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine za eneo la Asia Magharibi.

Ripoti iliyochapishwa katika chapisho la jana la gazeti hilo imefichua kuwa, maafisa wa Saudia wana wasiwasi mkubwa kuhusu hatari zinazokodolea macho uchumi wake kutokana na kuwa na uhusiano wa uhasama na taharuki na Tehran.

Ripoti hiyo imesema, "Mwenendo huu mpya wa Saudia wa kuona ni bora kuwa na uhusiano mzuri na mataifa ya eneo umetokana na hatua ya watawala wa Riyadh kutilia shaka uungaji mkono wa Marekani na waitifaki wake."

Gazeti hilo limewanukuu maafisa wa Saudia, Ulaya na Marekani waliothibitisha kuwa, wawakilishi wa Saudia na Iran wamekuwa na mawasiliano katika miezi ya hivi karibuni, kupitia nchi za Oman, Kuwait na Pakistan.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo The Wall Street Journal, Riyadh ililazimika kuangalia upya mahesabu yake, baada ya kushambuliwa vituo vyake vya kusafishia mafuta, hatua iliyoathiri uzalishaji wa mafuta nchini humo kwa asilimia 50.

Saudia na Marekani bila kutoa ushahidi wowote, ziliharakisha kuibua tuhuma kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imehusika katika mashambulizi hayo dhidi ya taasisi za mafuta zinazomilikiwa na Aramco.

Mashambulizi dhidi ya taasisi za mafuta za Aramco

Hata hivyo, siku chache zilizopita ripoti iliyotolewa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa Saudi Arabia ilisema kuwa, hawajapata ushahidi wa aina yoyote unaothibitisha kuwa Iran ilihusika na mashambulizi dhidi ya taasisi za mafuta za Saudi Arabia.

Itakumbukwa kuwa tarehe 14 Septemba mwaka huu 2019, Kikosi cha Ndege Zisizo na Rubani cha Jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi kilishambulia vituo vikubwa vya kusafisha mafuta vya Abqaiq na Khurais mashariki mwa Saudia ambavyo vinamilikiwa na shirika la Aramco. 

Tags

Maoni