Dec 15, 2019 01:11 UTC
  • Uchambuzi wa Sayyid Hassan Nasrullah kuhusu nafasi ya Marekani katika matukio ya Iraq na Lebanon

Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon juzi usiku alitoa hotuba kuhusu matukio ya karibuni huko Lebanon na katika eneo la Asia Magharibi.

Tokea maandamano ya Lebanon yaanze, msimamo imara wa Hizbullah na Katibu Mkuu wake umekuwa ni kuunga mkono matakwa ya wananchi na kupinga kujiuzulu serikali. Sayyid Hassan Nasrullah kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa ilikuwa kosa kujiuzulu serikali ikiwa  zimepita siku 45 tangu  Saad Hariri  ajiuzulu katika nafasi ya Waziri Mkuu wa Lebanon na kueleza kuwa kujiuzulu huko kulikuwa ni kupoteza wakati; hatua iliyosababisha kufungwa taasisi na idara muhimu za serikali. Wakati huo huo Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kuwa msimamo wa sasa wa Hizbullah ni kuunga mkono uundaji wa serikali pana itakayoyashirikisha makundi mbalimbali ya kisiasa huko Lebanon. 

Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon aliyejiuzulu 

Nukta muhimu ya pili katika hotuba ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ni kuhusu nafasi ya Marekani katika mchakato wa kuuandwa serikali mpya huko Lebanon. Kwa mtazamo wa Nasrullah, viongozi wa Marekani wamezidisha jitihada zao katika marhala hii kwa sababu kwa upande mmoja viongozi hao wanafanya juhudi ili kuundwa serikali mpya  ambayo itakwenda sambamba na maslahi ya Washington; na katika upande wa pili, viongozi hao wanadai kuwa Marekani inaisaidia Lebanon katika hali ambayo lengo la Marekani la kuisadia nchi hiyo ni kuitoa Hizbullah katika muundo wa kisiasa wa Lebanon. Ukweli ni kuwa viongozi wa Marekani wameunga mkono kujiuzulu serikali ya Hariri na hivi sasa wanatuma jumbe zisizo sahihi kwa wananchi wa Lebanon kwamba hali yao itaboreka iwapo Hizbullah itafutwa katika muundo wa madaraka wa nchi hiyo.  

Nukta muhimu ya tatu katika hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah ni sisitizo kuhusu hatua ya Marekani ya kuparamia wimbi la maandamano ya wananchi huko Lebanon na Iraq. Viongozi wa Marekani wamestafidi na mbinu mbili kuu katika maandamano hayo ya wananchi. Mbinu ya kwanza ni kuwa viongozi wa Washington wamejaribu kila wanaloweza kuwatumia mamluki wa ndani na wapinzani wa kisiasa ili kudhihirisha kuwa maandamano yanayoendelea huko Iraq na Lebanon hayasababishwi na malalamiko ya kimaisha ya wananchi bali ni ya kuipinga Iran. Sayyid Hassan Nasrullah ameeleza wazi kuhusu jambo hilo kwamba, maandamano ya Lebanon si ya kuipinga Iran na hakuna ishara yoyote pia kuhusu suala hilo. Amesema kinyume na madai ya viongozi wa Marekani; wananchi wa Lebanon wanaandamana kudai matwaka yao ya kiuchumi na kimaisha. 

Maandamano ya wananchi wa Iraq

Mbinu ya pili ya Marekani ni kuwa, viongozi wa nchi hiyo wanajaribu kila wawezalo kutumia vibaya maandamano hayo ya wananchi ili kuishinikiza Iran  ibadili siasa zake katika eneo hili. Hili ndilo lengo kuu la Marekani katika maandamano ya Lebanon na Iraq; na hiyo kuwa moja ya sababu kuu za kuendelea maandamano hayo.   

 Nukta ya nne  katika hotuba ya juzi ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ilikuwa kuhusu kutumia nguvu ya kieneo. Nukta hii iligawanyika katika sehemu mbili. Ya kwanza ni kuwa, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alieleza kuwa: "Tathmini kwamba Hizbullah ni hatari na tishio kwa maslahi ya Wazayuni ni sahihi. Sisi tunasema kwa fakhari kuwa ni tishio kwao." Pili ni kuwa, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa Iran haihitaji waitifaki wa kieneo kwa ajili ya kujilinda iwapo itashambuliwa, bali Iran yenyewe ndiyo itakayotoa jibu kwa shambulio lolote dhidi yake.  

Nukta ya mwisho ni hii kuwa matamshi ya Sayyid Hassan Nasrullah yanaonyesha kuwa viongozi wa Marekani na nchi waitifaki wao wanafuatilia malengo maalumu katika machafuko ya Lebanon na Iraq huku wakitaka kushadidishwa ghasi hizo dhidi ya raia katika nchi hizo huku wakiwatumia pia mamluki wao wa ndani kushadidisha hali ya mchafukoge katika eneo. 

Maoni