Dec 15, 2019 01:13 UTC
  • Harakati ya Answarullah ya Yemen: Marekani ndio inazuia kusimamishwa vita

Mohammed Ali al-Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen ameitaja Marekani kuwa ndio kizuizi kikuu cha kutosimamishwa uvamizi na mzingiro dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.

Akisisitiza kwamba uvamizi wa muungano wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen katika pande zote za nchi hiyo bado unaendelea, Ali al-Houthi ameongeza kwamba kuendelea mazungumzo ya amani katika mazingira ya sasa ni suala lisilowezekana. Aidha akibainisha kwamba muungano vamizi wa Saudia haujawahi kupiga hatua chanya kwa ajili ya kusimamisha uvamizi wake, amebainisha kwamba Yemen haipo tayari kufanya mazungumzo na nchi yoyote ile madamu uvamizi na mzingiro dhidi yake bado unaendelea. Kadhalika Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen amevitaja vikao vya hivi karibuni vya wakuu wa Baraza la Ushirikkiano la Ghuba ya Uajemi nchini Saudia dhidi ya Yemen kuwa ni vya uhasama na kusisitiza kuwa, taarifa ya mwisho ya vikao hivyo ni ushahidi tosha wa kupenda kujitanua kwa Saudia juu ya baraza hilo.

Mohammed Ali al-Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen

Itakumbukwa kuwa mkutano wa 40 wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ulifanyika siku ya Jumanne iliyopita huko Riyadh, mji mkuu wa Saudia. Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen, Mohammed Ali al-Houthi ameashiria suala la kushtadi tofauti kubwa kati ya Saudia na Imarati kuhusiana na Yemen na kusema kuwa, makubaliano ya Riyadh yalikuwa kiini macho, yasiyo na thamani yoyote na ambayo hayawezekani kutekelezwa. Saudia kwa kuungwa mkono na Marekani, Israel, Imarati na nchi nyingine za Kiarabu na za Magharibi ilianzisha mashambulizi yake makali dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 sambamba na kuizingira kila upande nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Tags

Maoni